Wednesday, July 23, 2014

WA NDOA NANI MWALIMU?




1
Ninamsaka mwalimu, Mwenye hasa uhitimu.
Mwalimu awe mwalimu, Wetu hata tuwe ndumu.

Kazi yao kwetu ngumu,Kuliko ya kuhukumu.
Wa ndoa nani mwalimu?
2
Sisemi wale walimu,Wenye maisha magumu.
Kwetu wao muhimu,Wazidi wao kudumu.
Tuache kuwahukumu,Ujira wao mgumu.
Wa ndoa nani mwalimu?
3
Wapo na pia walimu,Na wana zao elimu.
Lazima  tuwaheshimu,Daima pia wadumu.
Wanaweza kukirimu,Kwa Elimu maalumu.
Wa ndoa nani mwalimu?
4
Ramadhani na Swaumu,Wanamjua Imamu.
Irene na Adamu,Uchungaji wana hamu.
Daktari ni mwalimu,Puani usitoke damu.
Wa ndoa nani mwalimu?
5
Askari ni mwalimu,Kujihami ufahamu.
Mkandarasi kwangu mh!,Andiko sijafahamu.
Wahandishi ni walimu,Kwa wao utaalamu.
Wa ndoa nani mwalimu?


6
Mwizi ni mwalimu,Kwenye wake udhulumu.
Ili mradi ni elimu,Akupaye ni mwalimu.
Hata mapishi ya ndimu,Upo wake uhitimu
Wa ndoa nani mwalimu?
7
Wa vyeti ni ualimu,Wa Heshima u muhimu.
Wa darasa ualimu,Wa mtaa uheshimu.
Wa ibada ualimu, Wa nyumbani ualimu.
Wa ndoa nani mwalimu?
.8
Nadhani dawa muhimu, Si shule bali mwalimu.
Fikira azikhirimu, Afungue ufahamu.
Familia iwe dumu, Daima vichwa Timamu
Wa ndoa nani mwalimu?
9
Ndoani sana tudumu,Furaha japo kwa zamu.
Maisha yawe karamu, Upendo uwe kalamu.
Hekima pia Nidhamu, Nyumba isinuke damu.
Wa ndoa nani mwalimu?

10
Ndoa yakosa elimu, Digirii zetu sumu.
Twavuka nusu msimu, Twavuna hasi msimu.
Mama sitamlaumu, Baba mzamivu Sumu.
Wa ndoa nani mwalimu?

11
Muhimu sio Muhimu, Ujingani twajihimu.
Watoto kuwatuhumu,Kwanza tuwatibu Pumu
Ndoa yataka Elimu, Elimu Bora Elimu.
Wa ndoa nani mwalimu?

12
Tamati fika ni hamu, ghani hazinishi hamu.
Nina mengi ya muhimu,yahusuyo ualimu.
Wa ndoa nani mwalimu,kujua ni yangu hamu.
Wa ndoa nani mwalimu?










0 comments:

Post a Comment