Friday, December 20, 2013

Kiswahili ama Kiingereza? KISWAKINGE chatumeza.



 1
Sauti juu napaza, Ajibu mwenye uweza.
Nataka andika meza,Karibuni mboga Pweza
Wapishi wamekoloza, Tule bila ya kusaza.
Chumvi yetu kuongeza, Hilo hatutokataza.
Kachumbari tengeneza, Utamu usochukiza.
Ujinga si kuuliza,Uliza kwa kuuliza.
Kiswakinge Chatumeza, KingeHili Chatuuza
2
Kiingereza twaweza, Mwingereza Kapongeza?
Mmarekani azoza, ndio hasa Kiingereza?
Wakei wakikoreza, Wanaiji wakibeza?
Waghana hawajapoza, Waganda chawatukuza?
Wahindi wamejifunza, Wajepu kimewakuza?
Wachina wanakicheza, Wadochi wamekisaza?
Kiswakinge Chatumeza, KingeHili Chatuuza
3
Kiswahili tunoweza,Kulonga ama kuzoza?
Nahau tunazoweza, Mwilini zatutawaza?
Kiswahili mbele giza,Ung’eng’e una mwangaza?
Mazuri tuliyoweza, Ung’eng’e ndio mwangaza?
Farasi hatujaweza, Tembo hatujajiponza?
Ung’eng’e tuliomeza, Ni vipi utatukuza?
Kiswakinge Chatumeza, KingeHili Chatuuza
 
4
Twaona hili kengeza, kizazi twaangamiza.
Utashi tulopoteza, Ung’eng’e wadidimiza.
Misingi tunapoteza, Roho twaziangamiza.
Nyumbani tunapuuza, Ugeni tunatukuza.
Uzalendo unaoza, Dawa  si kiingereza.
Mdomoni chapendeza, Mifukoni chachuuza.
Kiswakinge Chatumeza, KingeHili Chatuuza
5
Undani wa lugha nini, Pengine  sijabaini.
Kuacha umasikini, Hekima lughani nini.
Busara si akilini, Akili ni busarani.
Chanzoni Umasikini, Kamsome Selemani.
Ung’eng’e sipingani, Undani nini sioni.
Kazi tulivu kundini, Amani chanzo lughani.
Kiswakinge Chatumeza, KingeHili Chatuuza
6
Zamani walibaini, Zamani yetu fanani.
Ubaberini Mnarani,Siri jueni lughani
Hatuwezi makumini, Tusikufuru mojani.
Tushikamane mwilini, Tugandane na rohoni.
Tuwe pamoja shuleni, Tusiachane shambani.
Relini hata lamini,Tufike wote angani.
Kiswakinge Chatumeza, KingeHili Chatuuza
7
Leo fasheni mbonini, Hatujui Ujombani.
Japo hatujulikani, Cheko zetu ung’eng’eni.
Usomi wa ujingani, Umeng’ang’ana rohoni.
Tajiri wa ung’ng’eni, Wanetu awape nini.
Na tuwatafakalini,Kwetu wanataka nini.
Sio  ung’eng’e jamani, Mafao kwao nyumbani.
Kiswakinge Chatumeza, KingeHili Chatuuza
8
Karibuni upwezani, Tupo hatujulikani.
Nchi tuilimbueni, Japo kiduchu mbeleni.
Uvunjaji hutuponi, Sifuri Uzalendoni.
Kiswahili ki porini, Hatunacho magegoni.
Twatusi familiani, Twatukuza ung’eng‘eni
Ung’ng’e u tabiani,Dawa anayo manani.
Kiswakinge Chatumeza, KingeHili Chatuuza


!!!!!!!!!!!!!!!!!!NAWAKUMBUKA NA WAKILISHA!!!!!!!!!!!!!!


























0 comments:

Post a Comment