Sunday, January 13, 2013

KATIBA MPYA YA TANZANIA


"chonde chonde, misingi,haki na wajibu vipewe kipaumbele"

 “MAAMUZI YETU NDIO HATIMA YETU”

Maoni kwenye katiba ni muhimu sana, na watanzania wote tulione hili kuwa ni jambo linalotuhusu sisi na vizazi vyetu, tuweke ITIKADI, JAZBA, KASUMBA(UBINAFSI) NA IDEOLOGIES zetu pembeni, na kuchangia kwa dhati ya kujenga taifa la Tanzania, la leo na kesho.Pia Serikali na Wahusika wote wa
mchakato mzima wa KATIBA, mtambue kuwa mmeshika dhamana ya watanzania wengi wa leo na kesho, mizimu yao itawafuata popote kama kwa makusudi mtu ataamua kufanya ama kusababisha MAKOSA katika hili! Wasomi Wetu,Makundi maalumu, Vyombo Vya Habari Na Wanasheria ambao ndio tegemeo letu kuu hapa hivyo hivyo,mizimu ya vizazi haitawaacha kwa kutotoa michango yenu wakati uwezo mnao,kwa sababu zisizo za Kitaifa/msingi! Wasanii wetu, kwa muda mrefu mmekuwa na malalamiko juu ya maslahi yenu ya kisanii, nafikiri ni wakati muafaka wa kuzitumia pia sanaa zenu kufikisha ujumbe maalumu wa maoni ya katiba, na pia kuisaidia jamii kuyafikisha maoni hayo,kwa kuwa wote tunaamini katika sauti ya sanaa katika jamii.

Tuache kulaumu tu, tushiriki kwenye zoezi hili, tusaidiane hata kwa kuelezea vizuri,kuna wanasheria wanaoweza kuelewa nilichosema na kukiweka katika muelekeo wa kikatiba,wasisite kufanya hivyo au kutoa mitazamo juu ya mchakato mzima kama kweli utatupelekea kufikia tunachohitaji? Mfano! Katiba itupatie vyakula bure! Je sentensi kama hii inajitosheleza au inahitaji maelezo zaidi?
Naamini wengi tutakachotoa ni hisia zetu na sio maoni ya kisheria,hivyo pengine hisia zetu zitapelekwa na kuchujwa kuwa kisheria, au kikatiba! Tunaamini, hakutakuwa na tofauti zaidi ya utashi wa lugha! Baadhi ya hisia hizo ni kama hizi kutoka Tankini! Kwa kufuatana na baadhi ya vipengere vilivyo kwenye katiba!

KWANZA HAPA MWANZONI TU KWENYE MISINGI

BADALA YA "KWA KUWA SISI Wananchi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tumeamua rasmi na kwa dhati kujenga katika nchi yetu jamii inayozingatia misingi ya uhuru, haki, udugu na amani":

Paongezewe maneno , UZALENDO,UMOJA,UHURU,HAKI,WAJIBU,UDUGU NA AMANI KWA MANUFAA YA TAIFA. Na nafikiri kuna umuhimu wa kuongeza Imani ya Taifa, hata tuseme ni 1. FIKRA BORA NDIO MSINGI WA MAENDELEO BORA 2. RASILIMALI ZETU NDIO UTU WETU 3.  MBELE YA MUNGU DAIMA WAMOJA

Hapa,pengine patatupatia muongozo wa  mtazamo na muonekano wetu kidunia. Na hii misingi ya Taifa iwe kweli misingi ya mtanzania na iwe hasa misingi ya viongozi wa Tanzania. Mfano: kama chama kinatoa sera, hata watanzania 50% waweze kuona sera hizo zinafaa vipi kwenye misingi na imani ya nchi! Tuweze kuwa na sababu ya kukubaliana au kukataliana, bila kugombana! Naamini kuna VICHWA vikali vinaweza kuliweka hili sawa kama linafaa.

MALENGO YA KATIBA

Lengo muhimu namba 9 kwenye katiba likao hivi

·         “Lengo la Katiba hii ni kuwezesha ujenzi wa Jamhuri ya Muungano na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar au wa chochote kati ya vyombo vyake na udugu na amani kutokana na kufuata siasa ya Ujamaa na Kujitegemea, amabyo inasisitiza
utekelezaji wa misingi ya kijamaa kwa kuzingatia mazingira yaliyomo katika Jamhuri ya Muungano. Kwa hiyo, Mamlaka ya Nchi na vyombo vyake vyote vinawajibika kuelekeza sera na shughuli zake zote katika lengo la kuhakikisha………………………….!”

LISOMEKE  HIVI
1.    Lengo la Katiba hii ni kuwezesha ujenzi wa Jamhuri ya Muungano na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar au wa chochote kati ya vyombo vyake na udugu na amani kutokana na kufuata siasa ya Ujamaa na Kujitegemea, ambayo inasisitiza utekelezaji wa misingi ya kijamaa kwa kuzingatia  mazingira yaliyomo katika Jamhuri ya Muungano. Kwa hiyo, Mamlaka ya Nchi na vyombo vyake vyote vinawajibika kuelekeza sera na shughuli zake zote katika lengo la kuhakikisha Inatumia Rasimali za nchi ili kusaidia Kulinda na Kukuza Tija ya  Rasilimali  zote za Nchi, Kupambana na Maradhi Nchini na Kukomesha Ufukara wa Watanzania Wote .

Pengine kutakuwa na maswali kadhaa juu ya mapendekezo haya. Kikubwa hapa ni mlengo wa kuhakikisha mwelekeo wetu uwe kuzithamini rasimali zetu na kuziboresha kwanza kabla hatujaona umuhimu wa kutumia za wenzetu. Imefika hatua sasa hata njiti za kutolea vyakula kwenye meno tunaona lazima zitoke nje, akitengeza mtanzania itakuwa haina UBORA.tatizo hilo! Ujamaa na Kujitegemea unakuwa wapi hapo!

Hata kitabu cha Kiswahili karibia kitakuwa bora cha kutoka nje,akiandika mtanzania hakina UBORA. Kama hiki kipengere kitakuwa ndio mtazamo wetu, ina maana, kila jambo la kitaifa litatakiwa kuhakiki kuwa mwisho wake linachangiaje katika hili. Kwa mfano, kama Serikali inapandisha mishahara ya Wafanyakazi, je kuna uhusiano gani na malengo haya?

Sio dhambi hata kidogo kuwa mzalendo, hata mungu anasisitiza kuwajali walio wa nyumbani kwako kabla ya yeye! Na sijui kama kuna mtu anaweza kutupatia uhakika wa kuwa watanzania wanapewa haki sawa na wageni kwenye nchi za ugenini. Tujue kusema kujipenda sio maana yake hatuwapendi wengine,bali tunawapenda kwa kadri inavyostahili.

MAMBO YA MUUNGANO

1.    Kiswahili kama lugha ya taifa kiwe ndio lugha ya kwanza kisheria kufundishia kuanzia ngazi ya shule ya msingi , Sekondari  mpaka Shahada ya kwanza, ikifuatiwa na Kiengereza. Kiswahili kiwe lazima  katika ofisi zote, Taasisi,Makampuni na Kwenye shughuli za biashara  kitaifa. Kiingereza kiwe lugha ya pili.Hili ndio lengo, lakini kutokana na ukweli kuwa hatuishi peke yetu duniani, tunahitaji kuwa na upeo mzuri wa kuweza kushirikiana na wenzetu. Hivyo tunahitaji lugha zao pia, hivyo basi kwenye marekebisho ya ndani, mfumo wa elimu unaweza kuruhusu, Kiingereza kutumika chekechea na shule za msingi. Kwa sababu, watoto ni wa watanzania wote na ni muhimu wapata msingi wa lugha hizo, na ni vema sana mtoto akifundishwa lugha hiyo wakati nyumbani anaendelea kufahamu kuongea kiswahili,na darasani anafundishwa Kiswahili fasaha.Kifupi ni kuwa lazima tuwe na utaratibu mahususi wa kuhakikisha kiswahili kinapewa uzito na kuelweka kwa kila mtanzania. Sasa, hata kama ndio Dunia inaongozwa na Kiingereza, hata Uraia,Historia yetu na Mengine hayawezi kufundishwa Kiswahili? Au basi hata kukifanya kuwa lazima kufundishwa Mpaka Shahada ya kwanza kama vile "Development Study" na "Communication Skills" kwa Mtanzania.

2.    Kiongezeke chombo kitakachosimamia Mwenendo na Ubora wa Rasilimali watu ya nchi.Ndani yake ndio kuwe na vitu kama Maadili ya Utumishi, Tafiti na Elimu! CHOMBO CHA KUSIMAMIA NA KUBORESHA  RASILIMALI WATU NCHINI

Kuna baadhi ya mambo huwezi kuyaona umuhimu wake mpaka yakuguse, fikiria mwanao kipenzi anapoonekana hafai katika kazi kwa sababu tu hajui Kiingereza wakati ofisi hiyo wanaoingia sana ni Watanzania, au unashindwa kuelewa mkataba kisa umeandikwa kiiengereza. Na hiyo ni mbali na mambo kama kutothaminiwa kwa waandishi wa vitabu wa Kiswahili,walimu, na mengine mengi ambayo hasa ndio yanaendana na malengo yetu makuu! (soma zaidi umuhimu wa lugha kwenye makala ya lugha: Kiswahili Muhimu kwa ubora wa Elimu Tanzania)

Serikali ina wataalamu wake, na vyombo vingine yaani Mahakama na Bunge! Vyote hivi huvutana na kushirikiana katika dhumuni la kuboresha yale yanayotakiwa na katiba, lakini nani mshauri huru wa hivi vyote au nani anayesema wewe unakosea hapa na huyu kakosea pale, au nani anasema anawawakilisha wananchi kusema majadiliano yenu yasisahau hili au lile! Sio mbaya kumpeleleza mpelelezi wako!

Tunahitaji kuwa na uwakilishi wa wataalamu usiofungamana na upande wowote, kama tuna wabunge wa kuteuliwa,sidhani kama itashindikana kuwapatia wataalamu nafasi chache za kuteuliwa kuhudhuria bunge ili kutoa mchango wa kitaalamu ambao upo kama sauti ya wataalamu wa Tanzania, na sio kwa ajili ya kuchangia au kurekebisha,bali kuboresha na kuongoza. Hapa tunaweza kupata undani wa wapi tumetoka,tulipo na tunakwenda kitaalamu. Kama taifa,serikali,vyama,wabunge na watanzania wanaweza kuona kwa undani hali ya nchi!

HAKI ZA MTANZANIA: IANDIKWE KUPATIWA
1.    Umiliki wa Ardhi na Makazi bora kwa kila mtanzania
2.    Elimu Bora mpaka ngazi ya shahada ya kwanza na ujuzi kwa kila mtanzania
3.    Mazingira bora ya kiafya (Matibabu na mengineyo kama haya)
4.    Chakula Bora
5.    Ajira na mafao ya ajira anapokuwa hajiwezi (Uzeeni na Ugonjwani)
6.    Miundombinu bora na Nyenzo bora  za msingi za kumuwezesha kupambana na mazingira katika ujenzi wa  Taifa,ikiwemo Lugha ya Kiswahili na ya Kiingereza.
7.    Kupata taarifa za maendeleo za siku,wiki mpaka mwaka juu ya mwenendo wa rasilimali za Taifa
8.    Kuhoji au kuhojiwa juu ya mapungufu au maboresho yahusuyo  maslahi ya umma
9.    Ulinzi wa kimwili na kisheria ili asibughudhiwe na mtu,watu ama taasisi yeyote anapokuwa katika kazi zake binafsi au za kitaifa nje ya utaratibu wa kisheria

Kwa kuwa hili ni gumu linapaswa kuwa ni lengo la kwanza, maana litakpokamilika, mambo mengi yatakuwa yamekamilika, nguvu zielekezwe huko. Serikali yetu ijue kuwa lazima impatie mtanzania mambo hayo ya msingi ili kuwa katika malengo ya Ujamaa na Kujitegemea. Kama Mihimili ya Nchi hailekezi macho kwenye haya, tutakuwa tunadanganyana. Tutakuwa tunaandaa maisha ya watanzania wachache huku tunasema ni kwa manufaa ya watanzania.

Kama ukipitia japo juu juu tu utagundua maoni mengi yanalenga sana mambo ya uraisi na vinginevyo! Sawa, lakini huko ni mwishoni,mzizi hasa uko kwenye hiziz haki za mtanzania, hata raisi atatakiwa kuangalia ni jinsi gani anatupatia hivi, au tuseme viko sawa? 
Na bila taarifa, ni vigumu saana kuwajibishana na rahisi sana kudanganyana,tuwe na utamaduni wa taarifa kutoka vitengo husika ili mahojiano yafanyike, mbona mabenki yanaweza?

WAJIBU WA MTANZANIA
1.     Kulipa na Kusaidia kukusanya kwa wakati Kodi zote Bila Kushurutishwa
2.     Kutii na Kuzijua sheria bila kushurutishwa
3.     Kulinda na kuheshimu Sheria za Nchi
4.     Kulinda nchi Kwa Nguvu na Aklili zako zote
5.     Kulinda na Kuheshimu Mali ya Umma kwa Nguvu  na Akili zako zote
6.     Kudumisha na Kuuboresha  Utanzania,Rasilimali za Tanzania, Miiko ya nchi na Utamaduni bora kwa nguvu na akili zako zote

Unataka haki wajibika kwanza. Kuanzia kwenye familia zetu,wengi ni mabingwa wa kulaumu kuliko kujilaumu! Ni mabingwa wa kutafuta sababu za kushindwa kuliko sababu za kufanikiwa! Ni wepesi wa kutetea ya kipuuzi kuliko ya maana. Na mengine mengi kama hayo

Kwa sasa watz hatujui hata kutofautisha HAKI,MSAADA NA WAJIBU.Ni kawaida hata mwanafunzi wa elimu ya juu kulaumu juu ya pesa kwa ajili ya simu ghali kuliko kujilaumu kutowahi darasani, au kutetea kutumia vibaya pesa aliyozidishiwa kuliko na kupinga kupewa kazi nyingi za kimasomo akiwa chuoni. Na hii mpaka kwenye utendaji wa serikali na Taasisi zake. Juhudi za kutambua uwajibikaji ni muhimu na kuboresha uwajibikaji ni muhimu saana Mfanyakazi bora kwa sasa ni kama sanaa ya kuigiza! Katiba ilione hili!

Leo hii Tanzania, utamaduni mzuri ni ule wa nje, usitegemee wa ndani kuendelea. Usafi wa mji ni jambo la halmashauri,raia wajibu wao ni kuchafua. Dereva halaumiwi mpaka ajali itokee! Sheria haifuatwi mpaka kuwe na hofu, na hofu ya kwanza iwe yetu wenyewe ndani ya mioyo yetu. Katiba ilione hili kuwa ni tatizo kubwa sana! itambue kuwa watz tunahitaji kupewa mazingira mazuri ili tutimize wajibu wetu kirahisi, na tusipo fanya hivyo, TUPATE STAHIKI YETU BARABARA!

MAMLAKA YA UMMA/BUNGE/MAMBO YA MUUNGANO
1.     Kuwe na chombo huru cha pamoja kwa ajili ya Mitazamo ya mwendo wa taifa kitaalamu, kitakachoundwa na vyombo huru kwa kubarikiwa na vyama vyote vya siasa nchinina wananchi kwa ujumla!

Imefika wakati sasa Tanzania kuongeza chombo ambacho kitakuwa na maoni ya kitaalamu bila kujali itikadi tulizonazo! Hapo yatapatikana mawazo ambayo kila mmoja wetu atakuwa na nafasi ya kuyachanganua na kuona kwa mtazamo wakitaifa. Kiwe na wawakilishi kwenye Vikao vya Bunge. Kitatokana na idara za tafiti,elimu ya juu na nyingine kama hizo! Hii ni kuboresha mitazamo ya kitaifa ili tunapokuwa na mpango basi uwe wetu wote na sio wa kundi fulani la nchi.

TUNAHITAJI CHOMBO AMBACHO KITAWAKUTANISHA WATAALAMU KUTOKA SEKTA ZOTE NA KUWA WANATUPEMBULIA PUMBA NA MCHELE.Kitatokana na CHOMBO CHA KUSIMAMIA NA KUBORESHA  RASILIMALI WATU NCHINI

Hebu fikiria kuwa hili swala la katiba lingekuwa limekuwa likifanyiwa kazi muda mrefu na watu waliobobea katika utaalamu wa sheria na siasa! Pengine kwa hivi sasa ingekuwa tunahakiki tu! Si kweli kuwa muda wa bunge unatosha kuyajadili na kuyaangalia kwa mapana mambo yote ya jamii yetu, ni mengi saana, na ndio maana mara nyingi tunaishia kubishana na kuiachia serikali kumalizia. Hata mnapokuwa kwenye mjadala mdogo tu, huwa ni vema wenye utashi na jambo hilo wakapewa uongozi wa mjadala, na wengine kuboresha, la sivyo mnaweza kufikia kuacha mchele mkachukua pumba. 

Katika mambo ya kitaifa chombo hiki kitawasaidia sio tu wananchi,bali hata wahusika wengine katika utendaji wao,mfano; kwa sasa tunajua shirika la nyumba linajenga nyumba, hivyo proposal zao kama zingepata mizani ya kutoka kwa wataalamu mbalimbali, hakutauwa na wa kulaumu kama mwananchi na kutakuwa na kusifia kutokana na kueleweka kwa jambo zuri linalofanywa hata kupinga wale wanaopenda kutuchanganya.


TOA MAONI  YA KIZALENDO

0 comments:

Post a Comment