Wednesday, February 27, 2013

MATOKEO YA KIDATO CHA NNE 2012-TANZANIA



 "LAWAMA HAZIJENGI, 
TUACHE KUENDEKEZA FIKRA MBOVU"

Ni vema kuanza kwa kujipa pole kama watanzania kwa mlipuko wa matokeo, ya kushangaza kiasi cha kufanya nchi na hata pengine Dunia kupigwa na butwaa! Maji yamekwisha mwagika, na hivyo ingekuwa vema mitandaoni kujae jinsi ya kutatua tatizo na sio maneno ya kashfa kwa viongozi na kunyoosheana vidole
!Kama ni Mchawi, basi ni karibu kila Mtanzania,na serikali yetu kama msimamizi mkuu wa mifumo ya Elimu,haiwezi kukwepa kuwa jalala!

Matokeo sio mazuri, na sababu zinaweza kuwa nyingi sana. Lakini mtazamo sahihi, pengine ungeanzia kwenye fikra zetu watanzania kwa ujumla. Je,kama wazazi  na walezi mitaani, tunawajika na familia zetu kwa kutoa miongozo sahihi na kukataza miongozo isiyo sawa? Viongozi wa Serikali, kwa nza kama wazazi wanawajibika ipasavyo katika eneo hili? Walimu wanawajibika ipasavyo katika eneo lao,japo kwa kiwango cha matatizo tuliyonayo? Na zaidi na kubwa kuliko yote ni je vijana wetu wenyewe, walau kunapokuwepo na uwajibikaji kutoka sehemu zingine japo kidogo, wao wanawajibika ipasavyo? Kwa kweli majibu ya haya maswali, karibu yote ni SIO, na kama NDIO, basi kwa kiwango kisicho SAWA. Na pengine kila mtu akiulizwa atatoa sababu ambazo ama zinakaribia ukweli au ni ukweli kabisa, na hakutakuwa na sababu ambayo si ya msingi. 

Kwa sasa, Wasomi wengi wa Tanzania, ukiwafuatilia, ni mabingwa sana wa kuiongelea serikali hasa kwa mabaya, lakini ukimuuliza, kutokana na upungufu huo umefanya nini kama msomi wa nchi hii, atakuambia serikali haisikilizi, au muda sina na kabisa anaweza kusema itaninufaisha nini mimi. Hiyo yote inaonyesha ni jinsi gani, hata elimu ya zamani ambayo wengi tunaipigia chepua kuwa ilikuwa bora, bado hatuitendei haki kwa maana ya kulisaidia Taifa hili, zaidi tunaitumia kama kwanza mkombozi wetu binafsi na kidogo serikali ikitaka, na sio mwananchi wa tanzania, ambaye kwa namna moja au nyingine ndie anayekutegemea sana. Hiyo tayari inaondoa kabisa maana ya Elimu Bora.Vivyo hivyo kwa wanafamilia wengi, watakwambia wako “busy” na maisha yao zaidi kiasi cha sio tu kuwasahau wadogo zao,bali hata watoto wao. Na kibaya zaidi ndio pale unapokuta wenye nafasi kubwa wengi katika jamii, wanashughulikia mambo yao, na zaidi mambo ambayo yanaendana na matakwa yao. Amini Usiamini madhara ya Bora Elimu ni mengi nchini mwetu na makubwa kuliko hata hili la matokeo ya Kidato cha Nne 2012.

Hakuna aliyelelewa na serikali ndio akapata juhudi,nidhamu,kujitambua, na heshima. Hata watoto yatima huwa wana walezi wao kambini. Serikali ilaumiwe kwa kutosaidia katika kurahisisha mafanikio ya mwananchi kwa kumpatia haki zake, zinazoweza kumfanya apate urahisi huo,hasa baada ya yeye pia kuwajibika ipasavyo. Mara nyingi tunaambiwa heshimu wazazi wako siku zako zipate kuwa nyingi duniani na upate mafanikio, nafikiri maana nyepesi ni kuwa WAZAZI ndio msingi wa kudumu. Yaani, familia, ikiwa na msingi mzuri, kuna nafasi kubwa ya vijana wake kupunguza SIFURI, sio tu darasani, bali hata mtaani,ambako hata wasomi wazuri kuna wakati wanachemsha. Hii, sio rahisi kuiona vizuri, lakini kulikuwa na msemo zamani kuwa mtoto wa mwalimu hawezi kufeli,sidhani kama ilikuwa kwa sababu ya mzazi kuwa mwalimu,bali ilikuwa ni kutokana na misingi ya walimu wengi wa nyakati hizo juu ya elimu! Ilikuwa ukiwa mtoto wa mwalimu unaweza kujuta, maana itakubidi uwe mfano, hivyo utasoma sana na kuchunga muda!

Sijui kama kwa sasa, mwalimu ana maisha mabaya zaidi ya wakati ule, lakini ninachoamini, ni kuwa mwalimu, hawezi kushindwa kumfundisha mtoto wake, kwa sababu serikali haimsikilizi! Mimi siwezi kufanya hilo,labda kama nina FIKRA MBOVU SANA. Lakini, naamini kabisa, kwa kutomtimizia mahitaji, yale yanayowezekana na yasiyowezekana, mwalimu, na kwa kutomsaidia mwalimu huyu kwenye madai yake dhidi ya serikali,sisi kama wazazi na jamii inayotambua umuhimu wa hilo, tunaweza kupelekea mwalimu akatafuta njia nyingine ya kutukumbusha, kama vile kutotoa mafunzo yaliyo bora. Akiwa anaamini kuwa baada ya matokeo mabovu, watanzania mtaungana naye katika kutatua matatizo. Nafikiri, huwezi kusoma gazeti ukakosa kusikia serikali ijali waalimu,tokea matokeo yatoke, na kuundwa kwa tume kutajitokeza hapo, wengine watapata umaarufu na wengine wataonesha kuwa walikwisha sema, na mambo kama hayo. Ni kawaida yetu kutatua matatizo baada ya kutokea, na ni kawaida yetu kupiga kelele sana tatizo likitokea na baada ya muda mfupi tu kusahau, bila hata kupata suluhu, na kuendelea kula bata tukisubiri lingine. Hizi ndio Fikra Mbovu, tulizojaaliwa! Hatuandiki, wala Hatusomi tutakumbuka vipi? Na ni mabingwa wa kuongea, kama hivi nifanyavyo mimi! Kudaaadeki!

Kelele zinazopigwa sasa juu ya matokea zingepigwa kuwasaidia walimu kwenye madai yao, naamini zingefanya kazi kubwa sana ya kupunguza zero leo. Kelele hizi, zingepigwa kuzuia matumizi mabaya ya technolojia na kuboresha matumizi mazuri ya technolojia, pengine zingetuondolea zero zingine. Kelele hizi zingepigwa kupinga FIKRA zozote zinazooneka kupotosha jamii, na kuitaka serikali iingilie kati, naamini zero kadhaa zingepungua. Na Kelele hizi zingepigwa na wasomi wanaochangia kwenye mitandao kuwarekebisha vijana na vyombo vya habari vinavyoonekana kuharibu FIKRA za jamii, naamini kabisa zero zingepungua. Kelele hizi zingepigwa kuwatambua watu wanaotoa mchango wa kuboresha jamii pia kwa namna yeyote, naamini kabisa vijana wengi wasingekubali kupata SIFURI leo. 

Kama jamii hatuwezi kuwa wazuri sana wa kuongelea mabaya ya serikali, na kujifanya kama hatuoni mapungufu yetu na watoto wetu. Sisi kama jamii tunapaswa kuisimamia elimu ya watoto wetu na kuiambia serikali wapi kuna matataizo na kuishinikiza kama tunavyoshinikiza mambo mengine.Kama Serikali imeachia soko huria Elimu na sisi tumeiachia serikali, maana yake tumewaacha vijana sokoni, na ndio maana vijana nao wanachagua kile ambacho kinawafaa kuwaingizia pesa haraka, na mara nyingi haiwezi kuwa elimu.Nguvu ya soko, inaonyesha Pesa zinapatikana kwenye Biashara na Sanaa na pengine kwenye  Saisa. Kwa hiyo vijana wataelekea huko pia,sasa ukileta habari ya mitihani, hata ningekuwa mimi zama hizi pengine ningepata zero tu! Naamka saa mbili, simuamkii mzazi, nalonga mpaka class, najadili na headphones, mwalimu ananiogopa na kachanganyikiwa na maisha,tuition kikubwa pesa, wasomi hawana hadhi kama wasanii, na mengine mengi kama ukata wa shule za kata, usipokuwa na ukakosa MUONGOZO WA FIKRA BORA hutoki kwenye ROUND ABOUT. 

Fikra mbovu, zinatupelekea leo hii, watu wanaona ukweli,lakini,wanaona wakisema hivyo,wataonekana wanaunga mkono chama tawala. Hivyo bora wakae kimya, maana wanaweza kuhatarisha maisha yao, jamii imekasirika, na sifa kubwa ya Mtu anayekuwa kwenye mapenzi na imani, ni wakati fulani kutoa maamuzi nje ya akili yake, na sheria itamsaidia,kwa kuwa alikuwa kichaa kwa muda, matokeo yake wewe uliyedhulika ndio umekula hasara! Utapata pole nyingi na kuombwa msamaha sana! Hebu, tumfikirie mtoto ambaye, kwa kuwepo sekondari ya kata, kapata hata nafasi ya kuona nini maana ya darasa la 12! Mtoto huyu, asingeweza hata kupata hiyo nafasi, lakini kwa mtazamo wa haraka, utaona kilicho karibu ni kulaumu kwa nini serikali haipeleki waalimu kule na mengine kibao, kama vile kuanzisha sekondari ile ilikuwa kosa kabisa! Naamini hata wakati shule binafsi zinataifishwa, kuna watu walipinga kwa kuona ubora utashuka, maana zitakuwa chini ya serikali yenye makosa asilimia 100%.

Matokeo ya Kidato cha nne mwaka huu, yatufanye tuweze kubadilika KIFIKRA na tuweze kuboresha elimu na sio tuzidi kulumbana na kuelekea kusiko sawa. Ya kufanyika yanaweza kuwa mengi kwa sababu mahitaji ni mengi, lakini Vipaumbele ni muhimu sana, pengine haya yanaweza kuwepo kwenye vipaumbele hivyo, na hasa kama wote tutaamua kubadilika KIFIKRA :
  1. Kuwe na kodi maalumu kwa ajili ya Elimu na Maslahi ya walimu tu kwa ngazi ya shule ya chekechea, msingi mpaka sekondari za serikali! Wataalamu wa uchumi, wekeni sawa hiyo!
  2. Kuwekwe Mfumo na sheria, ambayo jamii itakuwa ndio msimamizi mkuu wa ubora wa elimu, kama ambavyo jamii inahusishwa kwenye usimamizi wa rasilimali zingine za taifa. Hii itasaidia hata kuondoa kunyoosheana vidole kunapokuwa na tatizo! Ikiwa ni pamoja na  mfumo na sheria  ya kuwawajibisha  pia walimu na wazazi, kutokana na matokeo mabaya ya watoto wao! Na hata wanafunzi ikibidi!
  3. Kiingereza kitumike kama lugha ya kufundishia, kuanzia chekechea mpaka shule ya Msingi, wakati Sekondari mpaka ngazi ya Shahada ya Kwanza, Maofisi, Serikali na Binafsi na Mambo ya Kitaifa, Kiswahili kiwe lazima kama lugha ya kwanza, na Kiingereza kiwe lugha ya Pili! Na shahada za juu, Lugha yeyote iwe Ruksa, kulingana na mahitaji ya Vyuo!
  4. Tuwe na mkondo wa vipaji maalumu, mmoja tu,utakao simamiwa na serikali moja kwa moja na watoto hao kupata upendeleo, kuanzia chekechea mpaka elimu za juu!
  5. Tubadili miundo ya kutahini wanafunzi, Maendeleo ya kila siku yapewe kipaumbele kuliko mitihani, na yahusishe ushiriki wao katika jamii zaidi.
  Kama umesoma mpaka mwisho nakupongeza, maana ni dalili za kuwa na fikra bora! Kibongobongo, unasoma kichwa habari tu kama hakuna mambo yetu, unaipotezea!!!!!!



4 comments:

  1. Pamoja na mazuri Juma uliyagusia lakini nadhani ule Utanzania hatuna.Hivi tunatafsili nini maana ya serikali.Watu tumewachagua watuongoze ili tuwe tunasaidiana katika maamuzi lakini tunaona hao ndio kila kitu sio kweli.Wao wanaratibu maoni na mawazo yetu ili kuijenga nchi na sio kuamua kila kitu.Serikali ni sisi wote.Tuwe pamoja tutaweza kuijenga nchi.Watu hatuna uchungu na yetu.Hata wale ambao tunawategemea kuwa watatuongoza wakipewa nafasi pasipo na wasaidizi wazuri nao wanatoa madudu tu.Watanzania tunaendekeza siasa badala ya utendaji.Tangia tumalize uchaguzi 2010 ni kelele kila siku hatujatulia na kuanza kuangalia tufanye nini katika miaka hii mitano.Hebu tuangalie nchi kama USA na Uingereza utadhani kama hakukupita uchaguzi watu wapo busy na kazi.Jamani tutaondoka lini katika huu upofu na ujinga wa mawazo.
    Kuferi kwa wanafunzi leo msaada wangu kwako mzee ni huu;
    Tusiangalie na upande wa walimu tu hebu tuangalie je na wanafunzi nao wanapenda hiyo elimu?Enzi yetu mtu ukikosa kwenda sekondari unalia je leo ipo hivyo?
    Leo badala ya kulia mtoto analia mzazi kwa nn mwanae hapendi shule.
    Zamani usipoenda shule mbakora zinaanzia home mpaka shule je leo Mwl akimchapa mwanafunzi inakuwaje kwa mzazi
    Zamani kulikuwa na mchakamchaka na wanafunzi ukikimbia huwezi kuvaa chini ya matako a.k.a mlegezo lakini leo hakuna mchakamchaka.
    Zamani kulikuwa na mashindano ya kuimba mashairi,kutunga ngonjera,mashindano ya kiingereza na kulikuwa na minyororo kwa asiyezungumza kiingereza leo kuna mashindano ya kuhimiza matumizi ya kondomu ISHI, mashindano ya kuonyesha chupi
    Zamani kulikuwa na somo la ukakamavu na asubuhi kulikuwa na gwaride la wanafunzi wachafu leo hii kuna mashindano ya ukaguzi na mavazi ya vimini
    Zamani tuliwacheka wale wote wanaopenda masomo ya arts na kuwaona wadhaifu a.k.a masomo ya ngwini leo wote wanakimbilia huko.
    Zamani tulisoma masomo ya siasa lakini hakukuwepo na wanasiasa tulisoma ili tufauru leo hii siasa inaingilia hadi elimu.
    Zamani tulisoma ili tuwe madr.au maprofesa ili tuwe watafiti na mainjinia wazuri leo tunasoma ili tuwe wabunge.
    Zamani tunasoma ili tupate kazi leo hata ukisoma hupati kazi wanaajiriwa wenye fedha
    HIVI MNATEGEMEA NINI NA TUNATEGEMEA NINI KWA MTOTO ANAYEONA MZAZI WAKE KASOMA LAKINI HANA KITU WAKATI WAIMBA KWAYA WANAENDESHA MAVX-Fadhili Omari Cheo (MUST/INDIA)

    ReplyDelete
    Replies
    1. Serikali,tayari ina mengi ya kulaumiwa! na naamini hata wao wankubali,japo huwa hata wakifanya vizuri hatuwasifu! Sasa,mimi nafikiri kwa sasa dawa ni kutafuta suluhu ambazo haziongezi gharama sana serikalini, na zaidi ziwe zinatugusa wenyewe tunaoumia,maana mwanao akifeli,inakula kwako mzee!

      Delete
  2. bila kuwajibika hatufiki mbali, mtu akivurunda awajibike, kwa pamoja tutajenga Nchi. Angalia bandari wameanza kunyoka, TBS wameanza kunyoooka. Tuache ubabaishaji ktk hili. Mitaala hakuna, mishahara hafifu, nk. watu waachie ngazi. Atakayekuja atafanya kazi.

    ReplyDelete
  3. Ni kweli Kabisa! Kwa hiyo inawezekana, tatizo zaidi likawa ni nini katika hayo,maana nchi yetu tunaifahamu,kutatua yote kwa pamoja ni tatizo, kama mishahara hiyo ndio kabisa, utaambiwa labda baada ya uchaguzi! tunahitaji kupata ufumbuzi ambao unatibu matatizo mengi ili kupunguza gharama ya ufumbuzi!

    ReplyDelete