Monday, February 25, 2013

SIMBA SPORTS CLUBS - "Yaani mimi, Simba inapovurunda ndio naipenda sanaaaa!"



TUJENGE UWANJA KWANZA


TAIFA KUBWA 
NI


“MPIRA BORA KWANZA , MAGOLI, UBINGWA BAADAE”

USIYETAKA HILI HAMIA YANGA

Nakumbuka ilikuwa mwaka 1989, wakati naamini,ndio hasa nilipoweka sahihi ya kuwa nitakuwa mshabiki wa WEKUNDU MSIMBAZI MPAKA KUFA KWANGU. Hii ilikuwa ni baada ya kuwaona wachezaji kama Dan Mhoja, kama sikosei pia John Makelele akitokea benchi. Wengine Mtanisaidia mliokuwa
wakubwa kwa wakati huo.  Ilikuwa ni Uwanja wa MajiMaji Songea, na Nakumbuka Simba walilala kwa bao moja bila majibu, na goli hilo likifungwa na Mzee wa Kiminyio, Madaraka Suleimani.

Nasema niliweka Sahihi, kwa sababu, haikuwa mara ya kwanza kuisikia Simba au Yanga, na kuiona Majimaji au Tukuyu Stars kwa kuwa nilikuwa mwenyeji wa Mikoa hiyo miwili, yaani Ruvuma na Mbeya.Nilizipenda timu za nyumbani kama ada, lakini si kwa maumivu niliyoyapata kwa kufungwa Simba kwa siku ile. Naikumbuka Yanga, ikitoa Suluhu na Tukuyu Stars, kama sikosei mwaka 87, Abeid Mziba, akisawazisha dakika za mwisho kabisa, baada ya Marehemu Richard Lumumba kuwafunga Yanga mapema kabisa. Goli lilileta balaa kidogo kutokana na mpiga picha mmoja kuambulia kipigo kutoka kwa wachezaji wa Tukuyu Stars,kufuatia kutaka kumpiga Picha Golikipa Mbwana Makata. Ama kweli tayari ni Zamani sana!

Huwa najaribu kuangalia hasa kilichonifanya niipende Klabu hii ya Simba, naona sababu Kuu Mbili. Ya Kwanza, ni Kuwasikia wazazi wangu wakiiongelea kwa kuwa wao pia waliipenda sana klabu hii. Hii ilinifanya kupenda kusikiliza matangazo ya mpira na kufurahi sana hasa pale nilipokuwa nasikia majina ya wachezaji wa Simba, na kwa utoto wangu, Nakumbuka kusikia Iddi Pazi, Zuberi Magoha na Zamoyoni Mogella, Kisha ni GOOOOOOOOOOOOO! Na ya pili, ambayo nafikiri ndio kubwa sana kwangu ni ukweli kuwa aina ya mpira ambao ni asili ya Simba ni wa RADHA KWANZA,MAGOLI BAADAE. Hii kwangu mimi ndio furaha yangu. Na pengine ndio maana Wachezaji Kama Dani Mhoja,Selemeni Methew,Edward Chumila, Hussein Masha,Gaga,Ramadhani Leni Kasanga Bwalya wananichukua muda kidogo kuwasahau kirahisi. Hata Kwa Watani wangu wa Yanga, huwa ina nipa tabu kuona ni vipi mtu Kama Said Mwamba “Kizota”, Yusuph Macho,Method Mogella, Salvatory Edward,Steven Musa, Selestine “Sikinde” Mbunga na wengine wa namna hii ya uchezaji, walipenda kutumua muda wao katika Klabu hii Ya Jangwani.

Kuna mengi mazuri ya kuyakumbuka juu ya Simba, japo wengi watasema we mtoto wa juzi utatuambia nini, au we mshamba wa bara utatuambia nini, unaijulia wapi Simba, na maneno kama hayo ambayo ndio yamejaa vichwani mwetu watu wenye fikra mbovu. Washabiki wa Simba hatuwezi kuwa wote na umri sawa, au wote kuzaliwa Dar Es Salaam ama wote kushinda Msimbazi. Na sio rahisi kuwa wote, tuwe ni watoto wa wachezaji au tuwe tumewahi kuchezea Simba. Tunachoweza kukifanya kwa usawa ni Kuongea ukweli juu ya timu yetu,ili iendelee kutupatia furaha na raha tuliyoizoea. Kuipenda timu, sio kupiga sana kelele au kuvaa sana jezi na kupeperusha bendera asubuhi mpaka jioni, maana kama hivyo ndivyo,kila siku tungewaona wamiliki wa timu kubwa duniani, wakiwa na nguo zinazofanana na jezi za timu zao. Sio kwamba ukilia na machozi yakakutoka debe moja, ndio maana yake wewe ni mshabiki namba moja wa Simba,hata wanafiki huwa ni mabingwa wa kulia. Au sio mtu kwa sababu, una umri mkubwa na kadi yako ni ya zamani, basi wewe ndie mwenye uchungu sana na timu na mtu muhimu kuliko wengine,inawezekana kinachokuweka kwenye timu ni maslahi yako binafsi tu. Simba ni timu ya Wanaoipenda Simba, kuanzia watoto mpaka wazee, walio Tanzania na wasio Watanzania. Na mtu ukiwa na akili timamu hupaswi kucheza na kitu ambacho watu wanakipenda kama Simba, maana huleta laana ya kimaisha katika jamii hiyo. Nakumbuka na maneno ya Mjomba Wangu "Shibiki wa Yanga" Nassoro Kopa, aliwahi nihusia kuwa mpwa wangu popote duniani heshimu sana, Mapenzi, Mila na Imani, maana watu mara nyingi huwa na maamuzi ya bila kutumia akili, unapowakera katika mambo hayo. Unahitaji zaidi busara kuliko usomi unaposhughulikia maswala ya namna hiyo.

Kwangu mimi, kama kuna watu wanaweza kusema wenye Simba, na nikashindwa cha kuwajibu, basi ni familia ya Dewji,sijui hata kama wanauhusiono. Potelea mbali Uvumi uliosemwa juu ya matokeao ya dhidi ya “Stella Abdjani”mwaka 1993, lakini tulipata hata pa kuongelea, kama ni kufungwa fainali hata Bayern Munich wamefungwa kwao mara nyingi tu! Sio hivyo tu, mpaka leo naamini kuwa fainali ya ubingwa Afrika kati ya Enyimba na Ismailia mwaka 2003, ilipaswa kuwa kati ya Enyimba na Simba na pengine tungetwaa ubingwa wa Afrika, kwa sababu uwezo wa kuifunga enyimba ulikuwepo! Na nafikiri mpira ulitenda haki kabisa kumpatia Enyimba ubingwa ule. Jina la Mfadhili mkuu tena lilikuwa linaishia na Dewji. Ina maana Bila Kuishia Dewji mwishoni hatuwezi kufanya vizuri? Sidhani.Labda Kaseja anaweza kutuambia, Kuna nini Simba, Mpaka leo hii hatuwezi kuwa kama 2003?

Nimesema jina la Dewji, nikimaanisha hivyo, Simba Kali sana kwa umri wangu mimi bado ni ya POPADIC. Napo jina la mfadhili, mwishoni lilikuwa Dewji. Ulikuwa unaingia Uwanjani, huku unajiuliza tutashinda kuanzia 2 mpaka ngapi, na tutapigia mpira wa kiwango gani,hata wawe Pamba ya Mwanza, nini watani (YANGA), hawa ni wapinzani wa magoli, sio mpira. Mambo yalikuwa mazuri na tulicheka mwanzo wa mpira mpaka mwisho! Ndio Simba Sports Club inavyotakiwa kuwa, hatuongelei kuchukua kombe la Tanzania, isipokuwa TU kwa sababu ya kuweza kupata uwakilishi bora wa nchi yetu kwenye makombe ya KIMATAIFA. Sasa leo, mwaka sijui wa ngapi, radha hii sijaipata. Na kama sikosei, waliwahi ahidiwa watu, kupewa pesa kama wataifunga Simba. Haitoshi, wachezaji wengi walikwenda timu ya taifa na bado tuliweza kuendelea na ligi na kufanya vizuri. Sasa leo kidogo tu, inabidi tupumzike, wachezaji wetu warudi kutoka mechi za kimataifa. Simba inapaswa kuwa kitovu cha WATAALAMU wa kandanda Tanzania. Naamini, hata RADHA ya mpira wanayoishuhudia watu leo hii ya timu ya TAIFA inachangiwa sana na uwepo wa radha na ASILI ya mpira wa SIMBA SPORTS CLUB.

Wala sijasahau, maneno ya “METL”,akihojiwa na kituo kimoja cha Television nchini, alisema, kama wana Simba wako zaidi ya Milioni Kumi nchini, basi Simba ikiweza kuwafikia japo hao million kumi,inahitaji shilingi mia mbili kutoka kwa kila mmoja kuweza kununua uwanja wa Sigara,ambao kwa wakati huo walikuwa hawahitaji sana uwanja huo! Lakini kwa sababu, huwa sisi watanzania ni bora mtu utolewe jicho moja na jirani yako atolewe macho yote kuliko apata kitu kizuri mara mbili yako, tukaona yuko kwenye mpango wa kufaidika sana na timu ya Simba kuliko sisi wazawa wa nchi hii! Tukasahau yote aliyojitolea na kumtupia maneno ya hapa na pale, sisi akina nanihii, tuliozaliwa tunasema. Tokea aondoke sikumbuki kuwa na Simba kama ile,tena wachezaji wengi kutoka ndani ya nchi, na bado Hassan Hosam alikubali, baada ya kupigwa kanzu kwenye sita na mabeki wenye akili zao, Nampoka Nyumba na Pawasa, hiyo ndio Simba Yangu, RADHA KWANZA MAGOLI BAADAE kama BARCA na Liverpool . Sasa, jiwe tulilolikataa Simba linataka kuwa jiwe la msingi Jangwani na tayari ni jiwe la msingi Mbagala. Tujifunze kuwa,Kufanana sio undugu,ila kufaana.

Sipendi kuona timu ya Simba inakuwa tegemezi, lakini sipendi sana kuona timu ya Simba inakufa kimataifa, maana nilikwisha KINAI ushindi wa Simba dhidi ya Yanga au Prisons, nahitaji kuifunga Zamaleki na TP Mazembe,ili nikakipige na Barcelona. Napenda kuona mwanangu kama ana kipaji,anasoma shule ya Mpira wa Miguu inayoitwa “Taifa Kubwa..........”, na sio kuvaa jezi siku ya Simba na Yanga tu. Nahitaji kuona nalipa pesa kuingia uwanjani kuangalia mazoezi na kuwapokea wachezaji wa kimataifa, kwenye UWANJA wenye Geti Kubwa lenye maandishi, “SIMBA TAIFA KUBWA-NGUVU MOJA- MFALME MKALI DUNIANI”.Nahitaji, nikichoka nyumbani kwangu, niwashe television na kuanza kuona wachezaji wangu wa zamani,kama Pawasa, Matola,Ulimboka,Christopher, Nteze John Rungu, Masatu, Mwameja na wengine kibao wenye mauwezo ya kutisha, na kusikiliza WIMBO utakaonikumbusha wakati wa ujana wangu! Nahitaji mambo mengi sana, japo niyapate nikiwa kaburini! 

Sitaki kuona naulizwa, (Nchi za Nje), unapenda timu gani, nikijibu Simba,mtu anagusa Simu,halafu ananiambia Mbona Tanzania naiona Yanga au ndio Simba? Na Wala sitaki kusikia neno la utani “Timu haina hata Uwanja bwana”,hiyo timu au katimu. Sitaki kusikia maombi ya, mungu aisaidie Simba Huko Angola. Sitaki Kusikia Simba haina Timu ya vijana, au haijawalipa Vijana. Sitaki kuona Malumbano na Uongozi wangu yanatanda magazetini timu ikifungwa kidogo tu. Na wala sipendi kuona “tunabeep” mechi za kimataifa kama watani wetu, bora tuombe kuziuza nafasi mpaka tutakapokuwa tumejiandaa. Sitaki kuona kila uongozi ukibadilika basi kila kitu kinaanza upya,hadi kocha na usajili lazima vibadilike. Sitaki kuona kuna watu wanjifanya wenye Simba,wakati hata katiba haiwajui na wala hawajulikani has wapo kwa ajili ya nini kwenye timu. Na sitaki kuona Kamati ya ufundi haina Vigezo vya Kitaalamu. Sitaki Kuona Mambo mengi sana, naona niishie kusema sitaki kuona tunaendelea na ubabaishaji wa Kibongo, na kuifanya timu shamba la BIBI! Bora hata tuwe wa kumi miaka Ishirini kama Liverpool, lakini tunajua tunachokifanya kuliko kudanganyana kila mwaka nafasi za juu, kama Aghgh… halafu tunaishia kupata presha za kupanda na kushuka! Simba na Yanga, Utadhani tuna laana Fulani,hatuwezi kubadilika! Watani nao utashangaa katokea chizi,mambo yote yataharibika wawe kama sisi!

Jamani, Washabiki wa Simba tujiulize tunachokifanya, Sasa tunakokwenda ni tutapoteza hata uwezo wa kucheza mpira, kitu ambacho tunajivunia siku zote nchini. Swala kubwa lisiwe kulaumu uongozi au kuusifia kwa matokea ya uwanjani tu, kwa sasa viongozi wanajukumu kubwa moja tu kimsingi,la kujenga uwanja, SIMBA TUDAI UWANJA, na Viongozi wetu kwa sasa, wawe ni WENYE UWEZO WA KUTUONGOZA KUPATA UWANJA! Kufanya hivyo naamini kunahitaji mipango mikubwa ikiwemo kukata kabisa matumizi (Wengine tulipoona PHIRI anaondoka tulihisi ndio mipango yenyewe inaanza ya kukata matumizi),kuanzisha vyanzo vya pesa na kudhibiti pesa. Hii ndio rai yangu kwa Wanasimba. Na kwa Viongozi wa Simba, ujumbe wangu ni kuwa, tunahitaji uwanja, tunahitaji kudumisha aina yetu ya mpira na hadhi yetu ya kimataifa. Simba ni Timu Kubwa haya Mambo ya Kuishia kucheza Na Mtibwa Sisi hatujazoea, lakini Kwa sasa hebu na nyie iwaume kuwa Simba inaporomoka, tunaweza tusirudi tena katika ulimwengu wa soka maana vilabu vinazidi kuwa bora duniani. Usione raha,wakati wanasimba wanalia,kama kiongozi ujiulize unawaachia nini wanasimba? Utuachie kitu ambacho hata kihistoria kinashikika,sio makaratasini tu,mpaka mtu apekue ndio aseme huyu kiongozi alifanya hili! Tunataka, mtu akifungua tu Internet au gazeti miaka zaidi ya 50 baadae aone Ulichokifanya. Na ISIWE HAKA KAUBINGWA KA TANGANYIKA NDIO MTU UNAJIVUNIE, kiongozi yeyote anaweza kutwaa ubingwa huu kwa sasa, maana ni ubingwa wa Simba na Yanga.

Kuyapata haya, tunahitaji kitu cha kwanza, kuamua kama tunataka kuendelea kuwa wababishaji au tunabadilika. Mimi nashauri tubadilike, na hapo maana yake Viongozi wetu wawe wa kwanza kukubali kubadili mfumo, watuongooze kwenda kwenye mfumo wa uendeshaji soka wa kisasa,hata kama itatugharimu,basi ni vema itugharimu leo wakati tuna nusu shari. Jamani, tunaachwa sisi! Tuunde Misingi ya timu na kauli mbiu mpya,hata umoja wetu nao sasa ni kama umebaki kwenye nembo tu,hii ni kwa sababu wanasimba tunaanza kuwa Simba Ushindi tu, na mnaosababisha haya ni viongozi wetu,kwa sababu hamtutendei yale yanayoonekana. Angalia, tulivyofurahi kuona timu ya vijana ikifanya vizuri, nakucheza mpira wa asili yetu kabisa, kama timu kama ile ikidumishwa, hata msipochukua kombe miaka mitano, nani ataakulaumu kama baada ya hapo unacheza fainali ya Afrika? Kupigizana kelele na watu juu ya wachezaji wa nje, wakati tunahitaji pesa kukuza vipaji vyetu,haina maana, 1993 na 2003, kulikuwa na wachezaji wa nje wangapi? Wanachama tubadilike kwanza, na viongozi watabadilika tu, wanachama ndio tunao kuwa wapambe wa viongozi, na vigeugeu.Naamini, tukibadilika na kuwa wakweli na kuchagua asili yetu, tutapata uongozi mzuri, na tutaupa ushirikiano na utatunufaisha. Lakini tukiwa na tabia zetu hizi za kujipendekeza kwenye baadhi ya makundi ya wanaojiita wenye Simba, tutaishia kulumbana kwenye vitu vidogovidogo wakati vikubwa na vya msingi vinaharibika! Najua Kwa fikra mbovu, Mtu akisema Ukweli, Mtasema Yaanga Huyo! Ama wa ..........e huyo! Potelea Mbali,ila naamini kadi haijafutwa, naiweka hapa!
HATA ISHUKE DARAJA MI NAIPENDA TU!
HATA MNIFUKUZE MI NAIPENDA T!
HATA TUKOSE UBINGWA MI NAIPENDA TU!
  "Yaani mimi, Simba inapovurunda  ndio naipenda sanaaaa!"

4 comments:

  1. Umedorola juma wenzio tunapeta nyie mnaenda kuangalia mafuta wenzenu tunaenda kunusa Ulaya haaaaaaaaaaaaaaaaa

    ReplyDelete
    Replies
    1. Simba, wanaonekana kama wamedorola,ni kweli kwa kiasi fulani. Lakini,mtani na wewe uwe unajikagua,kwa miaka 8, ambayo umekuwa kati ya klabu zenye pesa pengine Africa,umefanya nini? au ndio ubingwa wa Africa mashariki,tulioubeba mara kibao hata bila hela mfukoni? Unatumia Milioni Mia Tano, kupata milioni 100, halafu unakuja kujisifia,kweli unaakili mtani! Si afadhali Simba tunakuuzia hata wachezaji, huku tunajikongoja. Simba wakipata hali uliyoipata miaka 8 iliyopita,wanachukua Kombe la Afrika hata bila UWANJA.

      Delete
  2. wajua shujaa si lazima aue simba ama adondoshe tembo hashaaa!ila fikra kama hizi zenye kutia chachu ya mapinduzi ya kweli ni ushujaa tosha asnante braaa!!LILA FAMILY,,,,,

    ReplyDelete
    Replies
    1. LILA! Nashukuru, maana hata nikifa baada ya miaka 50 ijayo,naamini maneno yangu hayatakufa,japo najua yatatumika zaidi na wenzetu wa nchi za nje,kwa sababu watanzania huwa hatusomi,na hata tunaposoma hatufiki mwisho, na tukifika mwisho huwa hatuwezi kurudia ili tuelewe vizuri.TUKO BUSY SANA HALAFU MASIKINI HATUENDELEI,SIJUI TATIZO NI NINI?

      Jitahidi,kubadilika LILA,usiwe kama sisi. Wahenga walinena,"NYUMBA BILA KITABU NI KAMA MWILI BILA ROHO".

      Delete