Sunday, March 17, 2013

JESHI LA KUJENGA TAIFA, LAZIMA?!! KIVIPI?!!



MPANGO WA LAZIMA KUPITIA JKT, HAUNA MASLAHI MAKUBWA KWA TAIFA LETU

NUKUU YA 1.  KUTOKA KWA DEUDATUS BALILE, 04 March 2013 09:45  “http://modans.go.tz/site/index.php/jeshi-la-kujenga-taifa-laagizwa-kuajiri-vijana-wa-kujitolea-“
 
Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi  Mhe. Dkt Jakaya Mrisho Kikwete ameliagiza Jeshi           la Kujenga Taifa (JKT) …………..Hayo aliyasema hivi karibuni alipotembelea  Makao     Makuu  ya  JKT,  jijini Dar es Salaam  ikiwa ni mara yake ya  kwanza  kwa  Makao Makuu             hayo kutembelewa na Rais  aliyeko madarakani tangu JKT ianzishwe mwaka 1963. 


“……Kwa Mujibu wa Meja Jenerali Muhuga uwezo wa kifedha uliopo ni mdogo     kuhudumia watu             katika kambi zote nchini, kinyume na ilivyokuwa JKT ya awali        kwamba wahitimu  wote wa kidato cha sita      wanajiunga na JKT kwa lazima. Hivyo kati ya            wahitimu zaidi ya 41,000 waliomaliza kidato hicho mwaka            2013 ni 5000 tu ndio   watajiunga kwa lazima na kutoka katika kundi  la hiyari la vijana pamoja na wabunge         47 watakaokuwa kambini kwa wiki tatu.
               
NUKUU YA 2.  KUTOKA     http://sabahionline.com/sw/articles/hoa/articles/features/2012/06/21/feature-02

Tanzania inajiandaa kurejesha mpango wa taifa wa jeshi la Kujenga Taifa, ambao ulisitishwa miaka 20…………….Pamoja na mafunzo ya kijeshi yenye kiwango, mpango huu pia hutoa mafunzo juu ya haki za binadamu, elimu ya uraia, na historia ya Tanganyika na zanzibar, na pia unakusudiwa kuamsha hisia za umoja na uzalendo kwa wanafunzi

Waziri wa Fedha wa Tanzania William Mgimwa aliliambia bunge wiki iliyopita kuwa kiasi cha shilingi bilioni 7.5 (dola milioni 4.7) zitatengwa katika bajeti ijayo ili kufufua mpango wa Jeshi la Kujenga Taifa.Kwa kuanzia, wanafunzi 5,000 tu wahitimu wa elimu ya juu watachaguliwa kushiriki katika mpango huo.

Waziri Mkuu wa zamani Edward Lowassa aliukaribisha uamuzi wa kuanzisha mpango huu, kwa kusema Jeshi la Kujenga Taifa liliwapa wanafunzi kutoka matabaka tofauti fursa ya kukaa pamoja kabla ya kujiunga na chuo kikuu na kujifunza kuhusu uzalendo na maadili ya Tanzania.
Alisema baadhi ya majirani wa Tanzania wameshindwa kufikia makubaliano katika nchi zao, jambo ambalo limechangiwa na kutokuwa kwao na utulivu. Tanzania imeweza kujitofautisha katika hilo kutokana na Jeshi la Kijenga Taifa, alisema.“Amani yetu haiwezi kutenganishwa na Jeshi la Kujenga Taifa,” Lowassa alisema. 

Kujenga kujiamini na kuimarisha umoja
Simon Mokiwa, mwenye umri wa miaka 42 na mkazi wa Dar es Salaam, ambaye alitumikia Jeshi la Kujenga Taifa katika kambi ya Bulombola Kigoma mwaka 1991, alisema shughuli hizo zilisaidia kujenga moyo wa ushindani na mtu kukabiliana na utofauti wa Tanzania. Mokiwa aliiambia Sabahi kuwa jeshi la Kujenga Taifa liliwasaidia vijana kujiamini wakati huo huo kujenga hisia za umoja.“Liliwaunganisha Watanzania wa asili mbali mbali,” alisema. “Wahindi, weupe na weusi walikwenda kambini, kufunzwa, kulima mashamba pamoja, bila ya kujali asili za familia zao. Nafikiri ni kitu kizuri kwa kizazi kipya na kwa taifa letu pia.”

Luteni kanali Hashim Mzava, afisa wa jeshi mstaafu, aliiambia Sabahi kuwa kufufuliwa kwa mpango wa Jeshi la Kujenga Taifa kutasaidia kuwajenga vijana na maadili mema ya kazi. “Watafunzwa mambo mengi kuhusu Tanzania na maslahi ya taifa. Haya hayafunzwi katika mtaala wa kawaida wa shule.”

Ikiwa serikali iko makini kuhusu kuugharimia mpango huu, lazima itenge pesa zaidi, alisema mwanauchumi Honest Ngowi.Ngowi, ambaye anafundisha katika Chuo Kikuu cha Maumbe, alisema wanafunzi 5,000 ambao sasa serikali imeshawapangia bajeti, ni sehemu tu ya wanafunzi 700,000 wanahitimu elimu ya juu kila mwaka.Ikiwa Watanzania wote watahitajika kushiriki katika mpango huu kabla ya kujiunga na chuo kikuu, lazima pesa nyingi zaidi ziingizwe ili kuuendeleza, alisema.

MWISHO WA KUNUKUU.
3.       KUTOKA TANKINI

Naipongeza serikali na wabunge wetu kwa kutambua kuwa kuna umuhimu wa kuwa tunathamini ZAMANI yetu Hili ni jambo jema na hasa pale tunapotambua kuwa uzalendo wan chi umeshuka, umoja unapotea na mambo mengi kama hayo ambayo yalikuwa nguzo kubwa sana katika kufikia hapa tulipo. Kwa kweli kuna mengi ya kujifunza na kuyaenzi kutokana na ZAMANI yetu. Lakini tunaisoma historia yetu ili iweze kutusaidia kuboresha leo na kesho,kulingana namazingira tuliyonayo. Ndio hasa tutapata faida ya HISTORIA na ZAMANI yetu.

Kwa kulitambua hilo, TANKI lina mchango TOFAUTI kwenye Maamuzi ya Kurudisha Utaratibu Wa Lazima kujiunga na Jeshi la Kujenga Taifa. JKT SIO MUHIMU KWA WATANZANIA WA LEO NA KESHO.

Wengi wa wachangiaji katika nukuu za hapo juu wameonekana kuamini kuwa Mpango huu utaturudishia Uzalendo Maadili, Umoja,Ukakamavu,Uvumilivu na kujenga msingi wa Amani. Japo bado hatukupewa ushahidi wa kitaalamu juu ya hili, naheshimu uzoefu wa watu walionukuliwa. 

ANGALIZO 1 : MABADILIKO TUTAENDANA NAYO?

Wakati umebadilika sana, mtoto wa miaka ya sitini, si sawa        kabisa na mtoto wa miaka ya tisini, na si sawa kabisa na mtoto wa miaka ya 2000. Sio tu kitabia, kimitazamo na kimahitaji bali hata kiafya. Ni watu wenye mazingira  tofauti       hata aina yao ya vyakula. Sijui kama uzoefu wetu unaweza kututhibitishia kuwa mafunzo ya jeshi yataliona hili. Au tutaombana tu msamaha pale mtoto tena wa dawa wa mtu akifariki kwa sababu ya        mchakamchaka, ambao hajawahi kukimbia tokea akiwa darasa la kwanza. Na Zamani, wengi walikuwa wanategemea elimu na kazi kutoka serikalini, na pengine ndio maana wakawa hawana ujanja juu ya jeshi. Lakini kwa sasa hivi, wakati mtoto kasomeshwa Uganda, chekechea, msingi Kenya, na Sekondari na chuo kamalizia India, akikataa kwenda jeshini,adhabu yake ni nini? Sio hivyo tu, miezi sita ambayo lazima apite jeshini,kama mzazi wake kapata nafasi ya kazi, inakuwaje,maana hatuna tena waajiri wa kusubiri umalize Jeshi. Kuna mengi pia juu ya Maadili na maana zake, kitaifa na kijamii. Sijui kama maadili tunayoyaongelewa hapa hapa ni yale ya kitaifa zaidi au pamoja na kijamii,ambayo kuna baadhi hupatiwa na wazazi wao kupitia aina Fulani ya mifumo kama ya Dini. 

ANGALIZO 2 : 

Amani kimsingi huambatana sana na haki. Sasa kwa kurudisha jeshi la kujenga taifa, tunaboreshaje misingi ya HAKI na haki zenyewe za mtanzania? Makundi mengi sana yanahitaji kutimiziwa haki zao,likiwemo kundi la MKULIMA, uwepo wa jeshi unaboreshaje haki yake? Kwa kuwaingilia vijana kwenye mipango yao ya kimaisha na kuwalazimisha kuwa lazima wapitie Jeshini, tunaboresha vipi haki hapo? Tusinywe dawa bila kujua ugonjwa, tunaweza kuongeza sumu mwilini. Amani ya Tanzania inahatarishwa na kasi ya kujitokeza kwa matabaka ya walio nacho na wasionacho. Amani ya Tanzania inahatarishwa na FIKRA MBOVU kwenye maeneo ya UWAJIBIKAJI, IMANI ZA DINI NA UZALENDO. Na wanaohatarisha amani ya Tanzania sio vijana kutoka matabaka ya WATANZANIA WA KAWAIDA, bali baadhi ya viongozi wa nchi na uwepo wa kundi kubwa la wanasiasa feki ambao kutwa ni kuhubiri juu ya mambo ya kichochezi na uongo kwa ajili ya maslahi yao. Jeshi litaweza kuyaondoa hayo kichwani mwa  kijana kwa muda wa miezi sita, au litamuongezea ujasiri wa kutetea fikra zake potofu kufa nakupona. Ama nalo jeshi litazidi kujenga matabaka kwa kuwafanya wasiopita jeshini kuwa raia feki.

ANGALIZO 3.

Bilioni 7.5, (yaani Kama vile Matreka safi 170) zimetengwa kwa ajili ya wanafunzi 5000 wa mwanzo, wakati wanaotakiwa ni (41,000). Na uzoefu mdogo niliona ni kuwa hizi pesa hazitatosha kwa hao 5000. Je, hizi pesa hasa zilitolewa kwa nani? Kodi ya Watanzania, ndio jibu sahihi. Je, kama tatizo lilisababisha kusitishwa kwa jeshi hili lilitokana na UKAPA, tayari kuna mahali sasa ambapo tutakuwa na uhakika wa kupata pesa bila kuyumba? Au ndio hidithi zile zile baada ya miaka miwili. Au uchumi sasa unakuwa kwa kasi kiasi cha kutuhakikishia kuwa na pesa hiyo bila wasiwasi.  Na hakuna ubishi kuwa jeshi lazima liwe la kiwango, maana vijana wa sasa ni wa kiwango na ukizingatia kutakuwa na mchanganyiko wa jinsia. La sivyo, ule ubovu wa maadili ndio utazidi na ununda utakuwa mara dufu. Mwanauchumi Ngowi hakutaka kuweka chumvi yeyote zaidi ya kusema kama Serikali inataka kufanya hilo lazima iandae pesa nyingi. Hii haiwezi kuwa ni sababu tosha kuona pengine serikali imeamua hili kisiasa zaidi? Maamuzi ya kisisasa kwenye mambo yanayogusa utaalamu mara nyingi huwa na madhara baada ya muda mrefu,tujiandae.

HITIMISHO LA TANKINI

Ni vema kila mtanzania anapokuwa na jambo la kuzungumzia kitaifa ajitahidi na kuweka hata kawazo kidogo. Uhuru wa kutoa mawazo ni mkubwa nchini mwetu na ndio wengine tunaishia kutukana viongozi wengi kitu ambacho sio sawa kabisa.

1.     TUBORESHE ELIMU YETU.
Yote tunayoyahitaji kwa dunia ya leo yanapatikana katika ELIMU BORA. Elimu bora huboresha fikra za mwananchi na kumpa upeo wa kuchanganua mambo kulingana na uhalisia wa mazingira aliyonayo. Serikali ianzishe KODI maalumu kwa ajili ya elimu na idhamilie kuweka misingi ya elimu bora. (Soma Makala ya Kuoberesha Elimu). 

2.     IMARISHA MAJESHI

Majeshi yako kibao Tanzania. JKT,TWTZ,POLISI,MAGEREZA,UHAMIAJI NA ZIMAMOTO. Haya yote yakipewa kipaumbele, yanatosha kuwa njia za kuwapatia wale WANAOTAKA kupitia majeshini, hizo nidhamu za jeshi kwa manufaa yao na ya kitaifa. Mpaka sasa hakuna Jeshi ambalo lina Askari wa kutosha. Hata uwiano wa askari na idadi ya wananchi pengine hautoshi, kitu ambacho maana yake haki ya ulinzi kwa watanzania na mali zao bado ina mapungufu sana. Kuboresha majeshi ni nguzo muhimu sana kwa maendeleo ya taifa. Kwa sasa jeshi kama la magereza nafikiri linaelekea kuwa linatia hasara taifa kuliko faida, wakati lilikuwa kati ya majeshi yanayoweza kujihudumia kwa kiasi kikubwa tu. Wape kipaumbele wanajeshi kwenye maeneo mbalimbali na kuwapa haki zao za kimaisha.

3.     BORESHA HAKI NA WAJIBU KWA WATANZANIA WA KAWAIDA.

Kitu cha muhimu kuwatanguliza watanzania kwenye kila jambo la kitaifa, na HII NDIO DHAMBI KUBWA INAYOWATAFUNA viongozi,serikali,wanasiasa wetu mlio wengi. Na itatafuna kizazi chetu chote, hata tukiwa kaburini. Tunachohubiri sio tulichonacho vichwani mwetu. Hatuwezi kukaa meza moja tukatafakari yahusuyo taifa, kisa hatuko CHAMA kimoja. Marufuku kumsifia mwenzio au kuchukua ushauri wake kisa, utachekwa umetumia sera za CHAMA kingine. Hatuwezi kusifiana pale tunafanya vizuri kwa sababu tu tuko vyama tofauti. Je huo ndio wajibu wetu kwa jamii yetu? Tokea tumetangaza MBIU ya Kilimo kwanza, mkulima wa jembe la mkono ameonja utamu wa kauli mbiu hii, na je wote tunaiunga mkono? Tunakumbusha ipasavyo na kushiriki kwa vitendo? Kata matumizi ya serikali yasiyo na umuhimu, tembea na wanyonge na lala nao majalalani uone kama uzalendo umekufa Tanzania. 

NAAMINI NA WEWE MZALENDO WA KWELI UNAYO YAKO, ONGEZA ILA;
“WENGI WAPE
NA
MBISHA WENGI MCHAWI”
“Tusiwe wajinga kama jamaa aliyekubali kufa aking'ng'nia kuwa dunia ni mviringo”

0 comments:

Post a Comment