Saturday, March 23, 2013

"MLALA HAI vs MLALA HOI"



 "MLALA HAI vs MLALA HOI".


Mlala HAI kasema,
Mlala HOI kubali.
Mlala hai kisima,

Mlala hoi  usali.
..............!

Kuna Michezo mingi Duniani ,kama vile Mpira wa Miguu na Ngumi. Mara nyingi michezo hii huwa ina muda maalumu, na taratibu fulani ambazo huwa zinapelekea kumalizika kwa mchezo na mshindi kupatikana, na  hat kupewa zawadi stahiki. Pindi ikitokea upande mmoja haukuridhika na maamuzi, mara nyingi hutokea vurugu ambazo husababisha madhara zaidi, sio tu kwa Timu iliyoshindwa, bali hata kwa ile timu iliyoshinda. Hili ni tatizo kubwa, ambalo sio tu vyombo vya michezo,bali sisi wote kama wahusika wa michezo hii,tunapaswa kulifahamu na kuangalia njia BORA ya kufikia matokeo ambayo wote tunaridhika..

Hata hivyo kuna baadhi ya mambo pia unaweza kuyafananisha na michezo hii. Mojawapo, ni mivutano baina ya MATABAKA katika jamii mbalimbali. Hapa hakuna muda maalumu na mshindi sio rahisi kusikia katangazwa, lakini kwa kuangalia dalali mtu anaweza kutambua mshindi ni nani. Kwa hiyo TANKI linapendekeza kuwa HUU ndio mchezo mgumu kuliko yote Duniani,ni vema basi tuweke sheria VIZURI ili mshindi awe anaridhika. Kwa kuwa, mpaka sasa hatuna sheria za mchezo huu, mechi nyingi tunaweza kutumia macho na akili zetu. MFANO:  TABAKA la WALALA HOI linaelemewa, hivyo ni bora hata kama sheria hazijapatikana, wajiandae kukubali matokeo ili kutoleta UGOMVI,ambao hautusaidii WOTE. YAANI:



"MLALA HAI vs MLALA HOI".

Mlala HAI ndarama,Mlala HOI dhalili.
Mlala hai kusoma,Mlala hoi  kauli.
Mlala hai kisima,Mlala hoi dhalili.
Mlala HAI kasema,Mlala HOI kubali.

Mlala hai tuhuma,Mlala hoi halali.
Mlala hai salama,Mlala hoi katili.
Mlala hai kasma,Mlala hoi medali.
Mlala HAI kasema,Mlala HOI kubali.

Mlala hoi ni sima,Mlala hai na wali.
MLala hoi na hema,Mlala hai na dali
Mlala hoi lazima,Mlala hai ni hali.
Mlala HAI kasema,Mlala HOI kubali.

Mlala hoi achama,Mlala hai awali.
Mlala hoi kachuma,Mlala hai dalali.
Mlala hoi kagema,Mlala hai kibali.
Mlala HAI kasema,Mlala HOI kubali.

Usijifanye  kusema,Usijifanye jabali.
Usijifanye kugoma,Usijifanye ni nduli.
Utajifanya we Umma,Utajifanya Ajali.
Mlala HAI kasema,Mlala HOI kubali.

Uyafanye yalo wema,Uyafanye ya Rosali.
Uyapende yake mwema,Uyapende ya kuswali.
Uyaongeze ya wema,Uyaongeze halali.
Mlala HAI kasema,Mlala HOI kubali.

Uyasake ya neema,Uyasake hata Mbali.
Ujue  yao ya Wema,Ujue ya Majabali.
Uwafae maamuma,Uwafae wa Akili.
Mlala HAI kasema,Mlala HOI kubali.

Uwe na walio nyuma,Uwe na walio Mbali.
Upende wanayosema,Upende kutoya swali.
Ukumbuke nayo sema,Ukumbuke kuyaswali.
Mlala HAI kasema,Mlala HOI kubali.

Dunia haina mwema,Dunia ya majabali.
Dunia ya Dhuluma,Dunia ya Baladhuli
Dunia mengi Lawama,Dunia mengi si Kweli.
Mlala HAI kasema,Mlala HOI kubali.

Duniani walo wema,Duniani hawang’ali.
Duniani nyingi homa,Duniani tuli huli.
Duniani nyingi njama,Duniani ni kabali.
MLALA HAI KASEMA,MLALA HOI KUBALI.

0 comments:

Post a Comment