Friday, April 12, 2013

TANGANYIKA NA ZANZIBARI

“ENYI WANANGU WAWILI, TANGANYIKA ZANZIBARI

Kweli mwanangu Akili, Hebu mwanangu fikiri.
Fiki mwanangu wa pili,Nawe mwanangu subiri.
Nyie wanangu wawili,Msifanye ya Bakiri.

ENYI WANANGU WAWILI,TANGANYIKA ZANZIBARI.

Kawa mwanangu Wakili, Kawa kiburi Bakiri.
Kawa mwanangu fedhuli, Kawa utu ufahari.
Hata muwe Wahadhili, Hakiwafai Kiburi.
ENYI WANANGU WAWILI, TANGANYIKA ZANZIBARI.

Haya yenu maadili, Mema kwenu nabashiri.
Japo hampo kamili,Mko wanangu  vizuri.
Wanangu msikalili,Mkawa ka’ matairi.
ENYI WANANGU WAWILI, TANGANYIKA ZANZIBARI.

Mzitumie akili,Msisahau fikiri.
Kukuza zenu akili,Msome bila kiburi.
Msiwe mabaladhuli,Msipende ufahari.
ENYI WANANGU WAWILI, TANGANYIKA ZANZIBARI.

Zisiwazidi akili,Zikawazidi  na shari.
Muwe na stahamili,Muwe na  kujihariri.
Mjenge na mihimili,Mpate na  utajiri.
ENYI WANANGU WAWILI, TANGANYIKA ZANZIBARI.

Asije kwenu Wakili,Na Amani ikithiri.
Ugomvi wenu wawili,Mwenzenu anasubiri.
Udini kwenu batili,Ukabila iwe shari.
ENYI WANANGU WAWILI, TANGANYIKA ZANZIBARI.

Kenya hata kule mbali,Msikilize habari.
Tanzania  Swali Sali,Swali Sali Zanzibari.
Dhulumu iwe batili,Isiwape utajiri.
ENYI WANANGU WAWILI, TANGANYIKA ZANZIBARI.

Ya moyoni yawe mbali,Ya akili yakithiri.
Akili ni muhimili,Akili tungi la shari.
Msijifanye viburi,Mkatupa ushauri.
ENYI WANANGU WAWILI, TANGANYIKA ZANZIBARI.

Hakuna kuwa kamili,Mpaka kwenye Kaburi.
Fikra nawe Akili,Muda hauwasubiri.
Jioni kwangu kamili,Maswali sitosubiri.
ENYI WANANGU WAWILI,TANGANYIKA ZANZIBARI.

0 comments:

Post a Comment