Saturday, July 6, 2013

KISWAHILI

„KISWAHILI Muhimili, Ni Roho mengine mwili“

Kiswahili Kiswahili, Hebu wote tujadili.
Vifimbo Cheza wa hili, Mudahili Umahili.
Daima tunajadili, Madini si Kiswahili.
 KISWAHILI Muhimili, Ni Roho mengine mwili .

Wengine tumekalili, Elimu si   Kiswahili.
Hawanayo afadhali, Magwiji wa Kiswahili.
Shahada juu ya mbili, Hawapewi ujabali.
KISWAHILI Muhimili, Ni Roho mengine mwili .

Hebu na tutafakali, Tena hata mara mbili.
Ung’eng’e tunakubali, Kiswahili kiko mbali.
Kivipi tufike mbali, Duniani wakubali?
KISWAHILI Muhimili, Ni Roho mengine mwili .

Sisi ndio Kiswahili, Ndio hasa wetu mwali.
Tumpende mara mbili, Wampende na wa mbali.
Watoe nyingi  Mahali, Sifaze zifike Mbali.
 KISWAHILI Muhimili, Ni Roho mengine mwili .

Kiswahili muhimili, Wasomi hawakubali.
Ubunifu uko mbali, Hatunayo kandambili.
Elimu Bora ni swali, Uzalendo uko Mbali.
KISWAHILI Muhimili, Ni Roho mengine mwili .

Wasomi wamekalili, Ung’eng’e ndio kamili.
Kiswahili si kamili, Sokoni hakishamili.
Soko lenye Majabali, Kipi chetu Muhimili?
KISWAHILI Muhimili, Ni Roho mengine mwili .

Msingi na wa Awali, Ung’eng’e si  Kiswahili.
Sekondari Kiswahili, Vyuo pia Kiswahili.
Ofisini Kiswahili, Binafsi na Serikali.
KISWAHILI Muhimili, Ni Roho mengine mwili .

Ung’eng’e usiwe mbali,  Na nduguze mbalibali.
Utufae kwa achali, Na pengine kwa ugali.
Lengo kuu Kiswahili, Kila ngazi kishamili.
KISWAHILI Muhimili, Ni Roho mengine mwili .

 Woga shida kukabili, Twaogopa na vivuli.
Sayansi labda kweli, Uraia sio kweli.
Ung’eng’e na Kiswahli, Lazima ni Kiswahili.
KISWAHILI Muhimili, Ni Roho mengine mwili .

Tunatupa Kiswahili, Tunabaki na LIMWILI.
Maroboti yana mwili, Yana pewa na Akili.
Fikiri mara ya Pili, Ufumbue  fumbo hili.
KISWAHILI Muhimili, Ni Roho mengine mwili .

0 comments:

Post a Comment