Tuesday, June 25, 2013

TULIANZA KUTUKANA, TUMEANZA KUPIGANA

"TULIANZA KUTUKANA, TUMEANZA KUPIGANA"

Imani nawe Amina, kama kesho kama jana.
Ugumba na wengi wana, neema za maulana.
Wote kwake nyie wana, ajua zenu amana.
TULIANZA KUTUKANA, TUMEANZA KUPIGANA.


Sitosema ya maana, sikufunzwa uugwana.
Nimejawa ya ujana, nimejazwa ya utwana.
Uzalendo mimi sina, mmimi mi mfitina.
TULIANZA KUTUKANA, TUMEANZA KUPIGANA.

Kwa sikio twapendana, kwa machoni twapingana
Kwa usoni ndugu wana, kwa moyoni twakanana.
Kwa ujinga twashikana, kwa ubora twagombana.
TULIANZA KUTUKANA, TUMEANZA KUPIGANA.

Ya akili tunayakana, ya moyo tunakabana.
Roho zetu zafanana, ya baba hurithi mwana.
Matendo mengi ya lana, si yale ya maulana.
TULIANZA KUTUKANA, TUMEANZA KUPIGANA.

Kura hazina maana, zinatupa tu fulana.
Hazilengi waungwana, wigo wake si mpana.
Wachache wenye maana,Kura huwala tena.
TULIANZA KUTUKANA, TUMEANZA KUPIGANA

Si kengere si adhana, Zana Pesa ndio dhana
Tumeitupa yetu jana, tumechagua fitina.
Busara yetu ya jana, leo si msingi tena.
TULIANZA KUTUKANA, TUMEANZA KUPIGANA

Tumeshindwa kujikana, hatuachi maulana.
Amani tumeikana, WAKILI tumpe jina.
Imetupata fitina, tusubiri kukandana.
TULIANZA KUTUKANA, TUMEANZA KUPIGANA

Roho kwatu twauana, hiyo sasa ni laana.
Adhabu ni zake Rabana, tiba zizile amana.
Hata kwa picha kuona, mafunzo tumeyakana..
TULIANZA KUTUKANA, TUMEANZA KUPIGANA

Ninakuomba Rabana,Uokoe wetu wana.
Waepushe na utwana, fikirani wawe wana.
Mali utu uwe dhana, pesa dhana waje kana
TULIANZA KUTUKANA, TUMEANZA KUPIGANA.

Asubuhi na mchana, kesho, leo hata jana.
Undugu si kufanana, Undugu ni kufaana.
Chagua yenye maana,  zingatia kwa maana.
TULIANZA KUTUKANA, TUMEANZA KUPIGANA.

0 comments:

Post a Comment