Sunday, August 25, 2013

"SHETANI ANATUTINGA"

Kabila langu Mkinga, Si Mkinga kwa kupinga
Machache mimi napinga, Hata kwa wangu Ujinga.
Mkono mimi napunga, Si Mafinga hata Mbinga
 MUUMBA TUNAMPINGA, SHETANI ANATUTINGA

Leo sisi tunaringa, Sheria tunazitunga.
Wachache wakizipinga, Maselo tunawafunga.
Sheria zenye ujinga, Kesho kwetu zitatinga.
MUUMBA TUNAMPINGA, SHETANI ANATUTINGA

Nayo nena ya kijinga, Mwelevu utayapinga.
Siasa yetu Ujinga, Hatuli wetu mpunga.
Mazuri inayapinga, Yang’ang’ania ujinga.
MUUMBA TUNAMPINGA, SHETANI ANATUTINGA

Demokrasia ujinga, Na wajinga wanaringa.
Busaraye naipinga, Pesa Ikulu natinga.
Nyoyo zenu nakonga, Ufalme weka nanga.
MUUMBA TUNAMPINGA, SHETANI ANATUTINGA

 Mifumo waliyojenga, Ubora sawa kuchunga.
Kwa bahati tunasonga,Hatusongi kwa kupanga.
Ubora tunautenga, Kwa uongo kuuchunga.
MUUMBA TUNAMPINGA, SHETANI ANATUTINGA

Utajiri watusonga, Akili tunazifunga.
Maadili tumepenga, Dini tunazipinga.
Halali tunazitwanga, Haramu tunazichunga
MUUMBA TUNAMPINGA, SHETANI ANATUTINGA

Mwisho wangu kupinga, Shauri mimi natunga.
Muumba kutompinga, Fikira tutazijenga.
Mazuri tutayapanga, Ujinga tutaupinga
MUUMBA TUNAMPINGA, SHETANI ANATUTINGA

Mifumo bila Ujinga,Tutaubonya mpunga.
Chekeche kama mchanga, Uchafu kutotuchenga.
Ubora uwe Upanga, Mifumoni kuujenga
MUUMBA TUNAMPINGA, SHETANI ANATUTINGA

Wewe nione mkinga, Ubishe haya kijinga.
Useme mimi napinga,Bila fikira kupanga.
Kesho mwisho wa kuringa, Muumba kaishapanga.
MUUMBA TUNAMPINGA, SHETANI ANATUTINGA

Muumba tumempinga, Shetani ndani katinga.
Mifumoni anaringa, hakuna wa kumpinga.
Machafu anayapanga, Wasafi  anawapinga
MUUMBA TUNAMPINGA, SHETANI ANATUTINGA

0 comments:

Post a Comment