Saturday, October 5, 2013

"ELIMU BORA MUHIMU"

1
Tunaipenda elimu, Na mimi ninayo hamu.
Si  hii Bora Elimu, Elimu ya usanamu.
Elimu Bora timamu, Bora Elimu Kuzimu.
Itufaayo Elimu,Si lazima ya kalamu.
Fikra Bora muhimu, Kuboresha Ufahamu
Makuu sio muhimu, Muhimu ndio Muhimu.
ELIMU BORA TIMAMU, HUYAMUDU MAJUKUMU.


2
Wa Elimu Bora elimu, Hayakwepi majukumu.
Wa Elimu Bora elimu, Huyajali ya muhimu.
Wa Elimu Bora elimu,Hajali tu kutuhumu.
Wa Bora Elimu elimu, Usimpe majukumu.
Wa Bora Elimu elimu,Ulafi amehitimu.
Wa Bora Elimu elimu,Jukumu ni udhulumu.
ELIMU BORA TIMAMU, HUYAMUDU MAJUKUMU.

3
Ya Bora Elimu elimu, Kwa jamii yetu sumu.
Ya Bora Elimu elimu, Yaua bora mabomu.
Ya Bora Elimu elimu,Yatubana bora pumu.
Ya juu Bora elimu, Si kitu bora chandimu.
Ya ng’mbo Bora elimu, Haina hata nidhamu.
Zamivu Bora elimu, Ni sifuri umuhimu.
ELIMU BORA TIMAMU, HUYAMUDU MAJUKUMU.

4
Ya mababu ni elimu, Ilifanya majukumu.
 Ya zamani ni elimu, Furaha  tele bila bumu!
Ukuu wake elimu, Majukumu ilikimu.
Madarasa si Elimu, Bila Kumudu jukumu.
Ung’eng’e sio Elimu,Japo ni chachu muhimu.
Kiswahili si Elimu, Kwa elimu ni muhimu.
ELIMU BORA TIMAMU, HUYAMUDU MAJUKUMU.

5
Leo Uongo Elimu, Kiungo chetu muhimu,
Wa mali na Wa Elimu, Wa mali ndio muhimu.
Ya watu ndio elimu, Ya kwetu hatuheshimu!
Uongozi gurudumu, Kilimo sio muhimu.
Ujanja kuvuta ndumu, Na uizi wa kalamu.
Ya leo ndio muhimu, Ya kesho si majukumu. 
ELIMU BORA TIMAMU, HUYAMUDU MAJUKUMU.

6
Tembea ona Elimu, Jakaya simlaumu.
Tandaa pata Elimu, Soma yaliyo muhimu.
Ongea pia salimu, Majungu sio muhimu.
Kujua mengi muhimu, Ng’amua bora muhimu.
Heshimu yao elimu, Heshima ndugu muhimu.
Zamani kuna Elimu, Wanyonge pia muhimu.
ELIMU BORA TIMAMU, HUYAMUDU MAJUKUMU.

7

Elimu Bora muhimu, Kuyamudu Majukumu.
Elimu Bora timamu, Muumba kesha kirimu.
Wachungaji Maimamu, Msaada ualimu.
Vitabu sio adimu, Welevu vichwani ndimu
Kesho nchini pagumu, Muumba simlaumu.
Twatupa yake Muhimu, Twakumbatia masumu.
ELIMU BORA TIMAMU, HUYAMUDU MAJUKUMU. 


8
Porojo kwetu muhimu, Porojo zenye Elimu.
Siasa Bora muhimu, Kuyamudu majukumu.
Sayansi Bora muhimu, Mazingira tuhukumu.
Fikira bora Muhimu, Utamaduni kudumu.
Uvumilivu muhimu, Kuvuka yetu magumu.
Akili zetu muhimu, Moyoni mengine sumu.
ELIMU BORA TIMAMU, HUYAMUDU MAJUKUMU.



.

0 comments:

Post a Comment