Sunday, October 13, 2013

Uzee siyo miaka

Uzee bado Kufika, Ujana unanicheka
1
Tokea  nimeamka, Mwenzenu nasononeka.
Jikoni kutosomeka, Heshima inatoweka.

Mtaa unanicheka, Kiangazi na masika.
Nyumbani wananicheka, Naonekana kibweka.
Nafunua nafunika, Hakuna ninachoshika.
Jioni inapofika, Matusi yanigubika.
Uzee bado Kufika, Ujana unanicheka
2
Nimeupiga mweleka, Fedha ninazikumbuka.
Niliringa na kucheka, Na kula bila kupika.
Machafu niliropoka, Dunia ikanichoka.
Ujanani nimedeka, Uzeeni sijafika.
Kwa ujinga nasifika, Welevu wananicheka.
Nijuacho  ni kusuka, Kwa marashi mi nanuka.
Uzee bado Kufika, Ujana unanicheka
3
Ukweli kutoutaka, Ni bora yangu hulka.
Uongo vema nashika, Ujinga mimi kiraka.
Kesi mbali ninaruka, Hakimu hutonishika.
Kwa jirani naitika,Kwa Mzazi ninafoka.
Marafiki nawasaka, Ndugu shida nawatwika.
Wapambe walinishika,Familia nalitoroka.
Uzee bado Kufika, Ujana unanicheka
4
Mengi ya kufikirika, Hakuna kukamilika.
Porojo zangu sifika, Vijiweni zatukuka.
Kitambi chanifumuka, Unyonyaji na kupoka.
Chozi latiririka, Ukweli nikikumbuka.
Ki hali nimenyauka, Ki mali nimekauka.
Hamsini sijavuka, Mkongojo nimeshika
Uzee bado Kufika, Ujana unanicheka
5
Najua  utanicheka, Fikira zikipofuka.
Zamani hutokumbuka, Mbeleni katu kufika
Dunia imewehuka, Shetani kishatuteka.
Jembe lako ndugu shika,kiangazi na masika.
Familia yako shika, Na nyumbani nanga weka.
Muda umekwishafika,Akili mbele kuweka
Uzee bado Kufika, Ujana unanicheka
6
Wanao ndugu kumbuka, Wasije ukawanuka.
Dunia akawateka, Jirani ulomcheka.
Asili yako kumbuka, Kubali umeumbuka.
Tambua umeanguka, Bora hukuvunjika.
Dira sasa ndugu shika, Dini Muhimu Kufika
Muda huwezi ushika, komaa na chakarika.
Uzee bado Kufika, Ujana unanicheka

7
Ujana ukikufika,Uzee Umekushika.
Ukikwepa  kutukuka,Uborani utafuka.
Waovu watakuruka, Wajinga kutokukuta.
Utoto ukiuruka,Uzee hujauvuka.
Hutajua pa kushika,Furahani hutofika
Mwilini utajanuka, Rohoni hutofufuka
Uzee bado Kufika, Ujana unanicheka
8
Uzee siyo miaka, Ujana sifa epuka.
Balehe ukiivuka, Majukumu ndugu shika.
Yako muhimu kumbuka, Acha zako patashika
Ninamuomba Rabuka, Mkono wangu kushika.
Wazazi wameondoka, Radhi zao sikutaka
Wanikana Tanganyika,  Wa Zenji nimewatoka
Uzee bado Kufika, Ujana unanicheka

0 comments:

Post a Comment