Saturday, January 25, 2014

Mama ataka msasa.



1
Uchungu kweli wa mama, Wa Baba sio wa mama.

Nyumbani hasa ni mama, Baba ubora ni mama.

Watoto hulia mama, Baba haiwi kiama.

Dira yetu kuu mama, Tangu Baba ni mzima.

Ujanani mwake mama, Aliuvaa umama.

Uzeeni kawa moma, Mama aleta zahama.

 Nyumba yaenda mrama,Mama ataka msasa


2

Sifa yake hasa mama, Ulezi sio unyama.

Huyu wetu sisi mama, twashaka kama mzima.

Itaja kesho zahama,Shangama yende mrama.

Koroboi anazima, Darasa eti kulima.

Marufuku kulalama, Hata tule bisi  sima.

Anaziponda ndarama, Na baba walizochuma.

Nyumba yaenda mrama,Mama ataka msasa


3

Ana yake moja kanga, Andiko BADO NATAMBA.

Kiswahiliche si Tanga,Kiswakinge ajilemba.

Haishi kutangatanga, Ala na kuhonga njemba.

Wanae kesho majanga, Tutamzidi kasumba.

Udumizi tutapanga,Hatutaweza jalamba.

Shetani kesha tutinga, Hatujui la muumba

Nyumba yaenda mrama,Mama ataka msasa
4

Usoni msafi mama, Rohoni hafai katu.

Utoto wetu kwa mama, Kwake hatujui kitu.

Atunywesha tui mama, Maziwa yote kwa watu.

Shidani tumwite mama, Rahani sisi vijitu.

Ukweni hagusi mama,Nyumbani hafiki mtu.

Ulezi hataki mama, Azoza na watu kitu.

Nyumba yaenda mrama,Mama ataka msasa


5

Mama yetu ni tapeli,Ajabu haibi mbali.

Nyumbani yeye jabali, Katiba kuponda mali.

Halindi rasilimali, hajali zake akili.

Anaunonesha mwili, Roho haipi wakili.

Imani sasa hajali, Amani kaibadili.

Mchana na kandambili,Usiku gari badili.

Mama aleta zahama, Nyumba yaenda mrama


6

Mama yetu anavisa, sijamaliza mikasa.

Naomba lenu darasa, Huyu wangu mama hasa?

Wengine kesha wanasa, Wanawe kwenye asusa.

Kichwani wampangusa,Asije akawasusa.

Ujinga wanamuasa, Azidi sisi tutosa.

Sitaki fanya makosa, Mimi mpiga msasa.

Nyumba yaenda mrama,Mama ataka msasa













2 comments:

  1. Mmmh kaka upo juu kwa mshairi I like it
    Allah akufanyie wepesi shule yako na.kila lenye kuwa jema kwako.

    Na akuepushe na kila baya
    asante sana kwa shairi kwangu nitajitahidi kuwa mama mzuri kwa familia.

    ReplyDelete
    Replies
    1. Nashukuru! Jitahidi, maana bila wewe hakuna kitu kwenda sawa! Wanao wataishia kugombana tu, mara umeme hakuna, mara wali hakuna, mara shule haendi, n.k

      Delete