Friday, January 31, 2014

MAMA ama MKE?

Kati ya mama na Mke,Kwanza namtibu Mke.

1
Swali lako Msafiri, Limenipa kufikiri.
Nimelipenda shairi, Hakika umehariri.
Linataka uhariri,Ujibu kwa kufikiri
Swali la kijemedari, Hujibiwa kijasiri
Usimkere Bashiri, Akuelewe na Shari.
Jibu tia zaatari,usikashifu Zaburi.
Kati ya mama na Mke,Kwanza namtibu Mke.
2
Vizingiti nimesoma, Mgonjwa mke na mama.
Mazingira umesema,Ama mke ama mama.
Hujataka kuchegama,Kwake mke kwake mama.
Wachache niliosoma,Wao bora hasa mama.
Sababu Nilizosoma, Ipo hofu ya kiama.
Wako pia walosema, Hupati mwingine mama.
Kati ya mama na Mke,Kwanza namtibu Mke.
3
Usidhani natania, Shairi kufurahia.
Wapo watofikiria, Limbwata lanizidia.
Wapo na wenzangu pia, Kupinga wanahofia.
Mke asikilizia, Mama anasubiria.
Kwa shida Ulimwambia,Haupo kwenye dunia.
Wabaya washangilia, Amuzi wasubiria.
Kati ya mama na Mke,Kwanza namtibu Mke.
4
Langu  liwazo chukua, Changanya zako chungua.
Mke ninayemjua, Hakuna chini ya jua.
Mama ulezi tambua, Huzuniyo huugua.
Ukishalionja jua, Mama ubibi kajua.
Ya muumba sijajua, Moyo wangu naujua.
Mkeo mwanangu jua,Akinuna naugua
Kati ya mama na Mke,Kwanza namtibu Mke.
5
Kudadavua karama, Anijalie karima.
Si Bora Mke kwa Mama, Kweli Mke Bora Mama
Kila mke hawi Mama, Hasa Mama ni umama.
Busara ina hekima,Lawama Bora kwa mama.
Laanani ukizama, Ya Mke sio ya mama.
Maafuu kwa Karima, Umama ni uadhama.
Kati ya mama na Mke,Kwanza namtibu Mke.

6
Tujadili kirafiki, Ye ndugu ama rafiki?
Mke kwa mama hafiki,Uzito upi havuki?

Wote sio wazandiki,Nani kwako mamluki?
Mkeo wammiliki,Kwa furaha ama dhiki?
Mke utamtaliki,Kwa Ndugu hutimliki?
Nani hasa mamluki, Mkeo ndugu rafiki? 
Kati ya mama na Mke,Kwanza namtibu Mke.

7
Changamoto umesema, Swali linayo hekima.
Kujibu sio lazima, Hata nje ya Kisima.
Wanaokwepa lawama, Mtu matendo nasema.
Uwe mke ama mama, Swali hili nawe soma.
Penye mke mume sema, Weka baba penye mama.
Kisha jibu nawe tuma, Kwa Zombe mwana Kisima.
Kati ya Baba na Mume,Kwanza Umtibu Mume?


 SWALI HILI HAPA
MAMA NAE WAKO MKE, UTAEMTIBU NANI?(CHANGAMOTO) - 30th Jan, 2014
Msafiri Zombe-Kisima cha Mashairi
( https://www.facebook.com/groups/Kisimamashairi/606837516053003/?notif_t=group_activity)

Mama nae wako mke, utaemtibu nani?

Mama ana ugonjwa wake, na mke maradhi flani

Utaemtibu mke? Au mama mzazi jamani?

Mama nae wako mke, utaemtibu nani?



Fedha haitoshi kabisa, kutibu wote wawili

Wote wanaumwa sasa, wanaikosa kauli

Nduguzo hawana pesa, ukweni zohofu ‘lhali

Mama nae wako mke, utaemtibu nani?



Pakukopa wewe huna, rafikizo wamechoka

Wagonjwa hali hawana, wanazidi kuteseka

Uwamuzi ulo maana, utoe pasi na shaka

Mama nae wako mke, utaemtibu nani?



Ni mama yako mzazi, anaumwa kweli kweli

Mke nae hajiwezi, hajitambui kwa hali

Wampenda wazi wazi, mke kwa yoyote hali

Mama nae wako mke, utaemtibu nani?



Umekaa miezi tisa, kwa wako mama tumboni

Umemtesa kabisa, malezi ya utotoni

Mke wamzoea sasa, mwingine wewe huoni

Mama nae wako mke, utaemtibu nani?



Ninaombeni majibu, utaemtibu nani?

Toa na zako sababu, hoja zako tubaini

Hali hii aghalabu, hutokea maishani

Mama nae wako mke, utaemtibu nani?

0 comments:

Post a Comment