Friday, February 21, 2014

MAJI YA KISIMANI,UTHAMANI FIKIRANI

Kisimani ni  Afya, Maji yakupe chafya.
Maji msingi wa Afya, Utu Bora si Afya.
Yatupe maji afya, Tuziache bofyabofya.

Leo zi nyingi chafya, Nyingi sio za afya.
Wanywa maji ya Afya, Uchafu mbele wabofya.
Utaikosa  afya,Kisima kitakubofya.
Maji yetu kisimani, Uthamani Fikirani.

Wengi nitawachekesha, Ujumbe sitofikisha.
Kuchapa mimi nakesha,Kusoma nilidondosha.
Mengi ninaaibisha, Hilo pia nitabisha.
Ukweli nababaisha, Uwongo nimewachosha.
Huwezi hodi kubisha, Nimefunga madirisha.
Jaribu kunikopesha, Ukome zangu gelesha.
Maji yetu kisimani, Uthamani Fikirani.

Fikira leo muhimu, Uzima  kesho kudumu.
Akili ziko za ndumu, Kama Roboti elimu.
Sio bora muhimu, Muhimu bora Muhimu.
Imani yangu timamu, Undani sijafahamu.
Uzima bora muhimu, Roho uje urahimu.
Ubora wake rajamu, Funua yake Rasimu.
Maji yetu kisimani, Uthamani Fikirani.

Nahisi naweweseka, Kisimani naumbuka.
Wachina bongo kufika,Maji yanabadilika.
Kisima kinajengeka,Maji bora ndio shaka.
Lumbano ni muafaka, Uborani kuongoka.
Mila isiyochujuka, Rohoni imevalika.
Bora fikira hulka,Kugoma kubadilika.
Maji yetu kisimani, Uthamani Fikirani.

Maji yetu kisimani,Lazima uwe makini.
Yapitie fikirani,Yaje kufaa mwilini.
Itupe yako imani, Tukutupe kaburini.
Muhimu bora ni nani, Mwenyeji ama mgeni.
Amini utabaini, Undani ni tamaduni.
Uboresho kisimani, Kuthamini tamaduni.
Maji yetu kisimani, Uthamani Fikirani.

Muumba kanijaalia,Kisimani kutulia.
Darasa nahudhuria, Majibu nasubiria.
Werevu unanijia, Ujinga wanirukia.
Ukweli unazo njia, Uwongo hutopitia.
Dunia inakimbia, Lughani tunasinzia.
Ukweli kwenye Dunia, Ni sifuri Zingatia.
Maji yetu kisimani, Uthamani Fikirani.

















 























0 comments:

Post a Comment