Wednesday, April 2, 2014

Mnyonge nyi mnyongeni,Na Haki yake Mpeni



1
Tumlaani shetani, Ubinafsi Shetani.
Hana mpango shambani, Maisha yake angani.
Akishuka aridhini, Atashinda tu majini

Maumivu kijijini,Mijini yahusu nini.
Swali la kutoka lini, Tajiri ajibu nini.
Tajiri afanye nini, Kitufae masikini.
Mnyonge tumnyongeni,La Hakiye tumpeni
2
Mkulima masikini, Uchumi wako ni nini?
Kushinda kwako shambani, Faida yake ni nini?
Jasho lako la shambani, Hasa laliwa na nani?
Maisha kwako ni nini, Useme u kivulini?
Unajipinda shambani, Wanakupunja sokoni.
Kilimo kwanza ni nini, Maumivu kilimoni?
Mnyonge tumnyongeni,La Hakiye tumpeni
3
Jadala kuu bungeni, Si kilimo ni madini.
Pembejeo si shambani, Zinaliwa tu mijini.
Ujanja sasa nchini,Siasani si shambani.
Mababu wawe shambani, Vijana jaa mijini.
Somo kilimo shuleni, Wanafunzi huwaoni.
Misaada kilimoni,Yaishia tafitini.
Mnyonge tumnyongeni,La Hakiye tumpeni
4

Wakulima vijijini, Hebu jamani semeni.
Mafao yao shambani, Mipango yafanya mboni.
Kodi zote ni shambani, Hadi simu mikononi.
Kuenda uraisini,Kura upate shambani.
Chakula kote nchini, Kinatoka Vijijini.
Wengi wetu wa mijini, Hasa kwetu vijijini.
Mnyonge tumnyongeni,La Hakiye tumpeni
5
Shambani ni vijijini, Mijini pia shambani
Ni wapi leo mjini, Hapakuwa kijijini?
Ufukara mashambani, Umasikini mijini
Waziri awe shambani, Ubunge si luningani.
Reli kufika shambani, Nchi iko duniani.
Waziri daladalani, Mboni yetu ya mijini.
Mnyonge tumnyongeni,La Hakiye tumpeni
6
Kilimo kikumbukeni, Mnyonge msitirini.
Jasho lao masikini, Wabungeni lioneni.
Wasomi wetu vyuoni, Mkulima mjueni.
Wataalamu nchini, Faida yenu ni nini?
Sayansi yetu jamani, Itufaacho ni nini?
Tuache ulimbukeni, Tujali kwetu nyumbani.
Mnyonge tumnyongeni,La Hakiye tumpeni

7


Elimu ziko mijini, Shambani abaki nani.
Shamba si usanii, Mkulima ale nini?
Wajanja si vijijini, Nakana huo Utani.
Wajinga wengi mijini, Tukibisha tubisheni.
Loliondo kumbukeni, Babu naye wa mjini?
Tamaduni tuthamini, Taaluma   zi shambani.
Mnyonge tumnyongeni,La Hakiye tumpeni





0 comments:

Post a Comment