Sunday, July 12, 2015

NATANGAZA YANGU NIA, URAISI KUUSHIKA.



1
NATANGAZA YANGU NIA, YA KWANGU KUWAFANYIA
FUNUNU NIMESIKIA, URAISI UNAWADIA.
SITAKI KUNIZUWIA,NI HAKI KWA MWENYE NIA.
MUHIMU NAULIZIA, KURA MTANIPATIA?
IKULU NAKIMBILIA, VINONO VILOBAKIA.
KWA RAHA NENDE JILIA, PASIPO MUULIZIA.
NATANGAZA KWENU NIA, URAISI NAUTAKA.

2
USIDHANI NI UTANI, UKANINYIMA SUKANI.
MWENZIO NIKO VITANI, KUKUONDOA GIZANI.
NATAKA UWE MAKINI, TONGO LITOKE MACHONI.
KUTOKA UFUKARANI, ONGOZO SIRINI NINI?
WAMKANA SELEMANI, SHIKA HATA UBUDHANI.
MENGI YANAYO THAMANI, YAMO PIA ANDIKONI.
NATANGAZA YANGU NIA,URAISI KUUSHIKA.

 3
MOJA NI CHAKULA BORA, HAKI HADI TORABORA.
SIHITAJI MAKOMBORA, TELE LIPO DONGO BORA.
TUNAZO FIKIRA BORA, LAZIMA NI MANYAPARA.
NIMEANDAA BAKORA, WATOLETA USAKARA.
HAITAKUWA MIKWARA, TUTASHINDIA MAPERA.
SOTE TUTASHINDA BARA, PWANI ZIBAKI BENDERA.
NATANGAZA YANGU NIA, URAISI KUUSHIKA.
4
AFYA BORA MUHIMU, HATA WAVUTAO NDUMU.
HAKUNA KITU KIGUMU, MUUMBA TUMLAUMU.
AKILI ZETU TIMAMU, DAWA ZIPO HATA NDIMU.
TUNAO WATAALAMU, TABIBU TUTAHESHIMU.
KALUMANZIRA MUHIMU, KWAKE BABU TUTADUMU.
SHUJAA AFIE HOME, HESHIMAYE ITADUMU.
NATANGAZA YANGU NIA,URAISI KUUSHIKA.

5
ELIMU TENA BALAA, SIO ELIMU YA VYETI.
USOMI UTAKOMAA, THAMANI VIPANDE VYETI.
LUGHA ISO NA LAGHAA, ELIMUNI KATIKATI.
UTASHI NJAA NJAA, HAPA UTASHIKA KOTI.
JAMII NI ULAMAA, AJUA ELIMU NYETI.
SAYANSINI TUTANGÁA, MUUMBA MBELE KWA DHATI.
NATANGAZA YANGU NIA, URAISI KUUSHIKA.
6
WANYONGE NA MSIHOFU, MALAZI KITU RAHISI.
MNATAKA MAJOKOFU, MHIFADHI FIRIGISI.
UMEME WA HITILAFU, TUMESEMA SASA BASI.
NANI ALO MTUKUFU, NANI SIO IBILISI.
MI SIGUSI SAKAFU, WE ULALIE SIAFU.
HAKUNA KWA WAONGOFU, WOTE MAKAZI YA NYASI.
NATANGAZA YANGU NIA, URAISI KUUSHIKA.

 7
DIRA JAMBO DOGO SANA, TUSILETE KUBISHANA.
TUTAFANYA KAZI BWANA, WATOTO WASOME SANA.
MAMA TUWAPENDE SANA, JAMII WALEE TENA.
DIRA ILO NA MAANA, WAZEE WAISHI SANA.
TUACHE KULA LAANA, NA PAKA WANONE SANA.
TUBURUDIKE KWA SANA, TUJIPUNGUZE KUNONA.
NATANGAZA YANGU NIA, URAISI KUUSHIKA.
8
KERO KUU YA AJIRA, NINAIJUA VIZURI.
HAITAKI MASIKHARA, NA HAITAKI KIBURI.
SITOZIGAWA AJIRA, HATA MSEME JEURI.
IPO DAWA BARABARA, WALA SIO YA TUNGURI.
MIUNDO MBINU IMARA, MISINGI YA WAAJIRI.
ISIISHIE MTWARA, WAIPATE IKWIRIRI.
NATANGAZA YANGU NIA, URAISI KUUSHIKA.

 9
AJIRA KWANGU NI HAKI, JAPO MAMA HATAMKI.
UCHOYO NA UNAFIKI, KUTWA NYUMA TUTABAKI.
UCHUMI WENU SITAKI, MATUMIZI SI RAFIKI.
UFUKARANI KUBAKI, UCHOYO NDIO KISIKI.
UKINUNUA MSWAKI, MWAKA KUTUPA HUTAKI.
UKARABATI WA LAKI, AJIRA ZIWE MALAKI?
NATANGAZA YANGU NIA, URAISI KUUSHIKA.

10
MIUNDO MBINU NI NGUZO, NI DAMU NDANI YA MWILI.
NCHINI TUNAUOZO, MUDA SISI HATUJALI.
FOLENI KUTWA GUMZO. SI DAR WALA MBALALI.
AKILI SANA TUNAZO, NI KUU RASILIMALI.
NINATOA MUONGOZO, NCHI ISAMBAE RELI.
PESA SIONI KIKWAZO, TUKIJIZILA MIILI.
NATANGAZA YANGU NIA, URAISI KUUSHIKA.

11
TAARIFA KUPUUZA, HATARI NIMEGUNDUA.
NCHI TUTAJA IUZA, TUBAKIE NA MAPUA.
HAPA SAUTI NAPAZA, HAKI YAKO ZITAKUA.
ZISISUBIRI BARAZA, MABAYA KUYAFUKUA.
ZIYACHUJE MAVILAZA, UJINGA UJE PUNGUA
ZIHOJI NA KUCHUNGUZA, UMMA USIJE UNGUA.
NATANGAZA YANGU NIA, URAISI KUUSHIKA.
12
ARDHI SINA UBISHI, KILA MTU MMILIKI.
SITOLAMBA MATAPISHI, SHERIA SIIMILIKI.
KATIBA SI MATAMSHI, KIVIPI HATUANDIKI.
MILELE SIWEZI ISHI, NCHI VIPI NIMILIKI.
WENGI HATUNA UTASHI, NI KIPI HASA NI HAKI.
SITOLETA MAGUMASHI, HII YAKO KURA HAKI.
NATANGAZA YANGU NIA, URAISI KUUSHIKA.

13
WAJIBU HAKIYE KAZI, KAZI NDIO WETU UTU.
KIPATO HAKI YA KAZI, VIPI ANALIPWA MTU?
KAZI ZILIPE WAKAZI, PESA SI KITU CHA MTU.
UZALENDO NDIO NGAZI, KODI HAKI YAKE MTU.
NIKISHINDA LA UWAZI, LA GIZANI SIO KITU.
MAENDELEO NA KAZI, NI KAMA MOYO NA MTU.
NATANGAZA YANGU NIA, URAISI KUUSHIKA.

14
UFISADI NDIO NGOMA, WATOTO HAIWAHUSU.
HILI NINAYO HEKIMA, KWA NDANI NIMEDURURSU.
TUSIJE MTUSI MAMA, HAYUPO HATUPO NUSU.
MAFISADI KWELI NOMA, TANDAO LAO SI NUSU.
HAKIMU ZINGIRA SOMA, DAWA SIO MAHABUSU.
MAJIMBO KWAO NI HOMA, FILISI NI LAO BUSU.
NATANGAZA YANGU NIA, URAISI KUUSHIKA.

15
RUSHWA NDOGO SIO HOMA, HAITABAKI KIGOMA.
HATUITAKI DODOMA, IMELETA TRAKOMA.
DAWAYE IPO KWA MAMA, VITABU TUKIVISOMA.
UWAZI MSINGI MWEMA, TUSIJE KWEPA LAWAMA.
HAKUNA JELA NASEMA, YATUACHIA ULEMA.
MIFUMO FEKI UKOMA,HABARI ZINACHUTAMA.
NATANGAZA YANGU NIA, URAISI KUUSHIKA.
16
KATIBA KWANGU NI BABA, AMPENDAYE NA MAMA.
HAFANYI MCHEZO BABA, NYUMBA IENDE MRAMA.
ATULINDE SANA BABA, HAPENDI BURE KUHEMA.
UTAMBULISHO NI BABA, MSINGI BORA UMAMA.
UBORA WAKE KATIBA, KUTHAMINI TAALUMA.
WAJIBU NA HAKI TIBA, UBINAFSI UNYAMA.
NATANGAZA YANGU NIA, URAISI KUUSHIKA.

17
MATEJA NYIE WANANGU, VIPI NIJE WASAHAU.
PENGINE APENDE MUNGU, PIPI ZIWE KAUKAU.
TAIFA LISILO MUNGU, WANAWE LITASAHAU.
MWANA AKILAMBA CHUNGU,CHACHU KATU HASAHAU.
SHIKENI HILI LA KWANGU, MADAWA MTASAHAU.
SITAKI MIA MIZUNGU, NITAWAFANYA WADAU.
NATANGAZA YANGU NIA, URAISI KUUSHIKA.
18
WALE DADA ZANGU POA, UKOMBOZI SIJALETA.
NAANZA NA KAKAPOA, NYIE HASA NDO WATATA.
HAKI YAO NITATOA, YA KIFO YAO WATATA.
HILO GONJWA SIO POA, JAMII IKILIPATA.
KARANTINI NITATOA, MATIBABU WATAPATA.
NAJUA WANATUBOA, HEKIMAYE PIA TATA.
NATANGAZA YANGU NIA, URAISI KUUSHIKA.

19
NATANGAZA YANGU NIA, KILIMO KUKIKOMBOA.
MKULIMA YANGU NIA, LANGU TAMKO NATOA
DIRA BORA TANZANIA, MKULIMA KUMTOA.
ELIMU BORA NI NJIA,MKULIMA KUTOBOA.
MAKAZI YALOTULIA,TUSIPATE KUKOHOA.
DAWA TEKNOLOJIA, SIYO YA KUJIPODOA
NATANGAZA YANGU NIA, URAISI KUUSHIKA.

20
KATIBA NINARUDIA,UMUHIMU NAUJUA.
IKULU NIKIINGIA, CHA KWANZA NIMECHAGUA
KATIBA YA TANZANIA, WAANDIKE WANOJUA.
MTAWALA NILO MIA, HAKIKA MTANIJUA.
SIACHI KUSIMAMIA, MKULIMA ASOJUA.
KATIBA NITATUMIA, MTUMWA ALOAMUA.
NATANGAZA YANGU NIA, URAISI KUUSHIKA.

0 comments:

Post a Comment