MAFANIKIO BORA YANAHITAJI MIPANGO BORA KWANZA
Umuhimu wa mipango bora kwanza |
Ukiona vinaelea Ujue vimeundwa. Ni kama kusema mambo mengi mazuri hutokana na kuumiza kichwa "Fikra Bora". Au Kupanga Kwanza ndio Msingi wa mafanikio. Kwa kweli Kubahatisha mafanikio katika
Dunia ya sasa na ijayo ni nadra sana. Tuamue kutegemea kubahatisha au kuumiza vichwa na Kupanga kwa usahihi na Kusimamia Kwa usahihi, maana, ndugu wa karibu sana wa kupanga ni kusimamia. Baadhi ya majengo pembeni ya Mto maarufu wa Rhine-Koln |
Umefika wakati sasa sisi wananchi na viongozi wetu tuliweke hilo mbele. Tujue kuwa ujanjaujanja mwingi mbele wote tunaweza kuwa gizani na asitokee hata mmoja wetu akawa na unafuu kama ambavyo pengine wengine wanategemea.Tuchague, kama mwalimu Nyerere alivyotuambia kuwa kupanga ni kuchagua,tujifunze kuchagua ya kuyafanya na ya kuyaacha kwanza. Kwenye Kupanga kunahitaji utashi wa hali ya juu,maana ni lazima kuumiza kichwa na kuingalia njia yote ya kule uendako, hivyo ni lazima tujue kuwa sio wote tuna vichwa vya kuweza kupanga kwa ajili ya nchi. Hivyo basi, tuheshimu na kuwapa nafasi wataalamu wetu ili waweze kuonyesha njia,wengine sisi tuwe tu wakaguzi wa uhalisia wa njia hizo. Na lazima wataalamu wetu wapewe nafasi ya kutupatia mipango bora sio hii ya bora mipango yenye ujanjaujanja wa kutupiga machanga ya macho. Wataalamu tunao, ila tatizo ni kuwapata na kuwatumia vizuri. Hapo ndio kazi kwelikweli, kwa sababu ya muingiliano wa kiitikadi na mitazamo huwa mara nyingine tunawapata na kuwatumia vibaya, au hatuwapati waliobora. Tuweke utaifa mbele kwanza,tukubali ukweli tutapata wataalamu sahihi kabisa. Kumbuka Kizuri chajiuza,kibaya chajitembeza na hivyo ni rahisi kukipata.
Daraja la Matreni Kuelekea kituo kikuu cha usafiri-Koln |
Tusiwe watumwa wa maendeleo ya wenzetu bila kujua walifikiaje walipo. Unaweza kufikia alipofika mwenzio ndani ya muda mfupi,lakini huwezi kufikia bila kuumia zaidi ya alivyoumia yeye, utakuwa umebahatisha au umedhulumu.Njia ambazo si sawa. Siku zote lazima uamue hata katika familia, Mheshimiwa Mkapa aliwahi sema,tukubaliane kula mpaka chakula cha watoto wetu,ama tuishi kwa kujibana ili walau wanetu waje kukikuta chakula chao! Wazazi katika nyumba huamua hivyohivyo, walale njaa,watoto waende shule au wanywee zote mambo baadae yatajiendesha? Hapo huwa panatakiwa kuumiza kichwa na hasa ndio penye Ubaba na Umama.
Treni zikiingia kituo kikuu,tunaweza kuwafikia kama tukibadilika kifikra |
Msanii wa kizazi kipya Fid Q "dedication to my son Feisal",anasema ni rahisi kuwa baba mzazi,lakini ni kazi sana kuwa BABA, kwa sababu hilo linahitaji muongozo safi, utashi na kukidhi mahitaji. Yaani uwezo wa kufikiri na kutekeleza yote ambayo BABA anatarajiwa kuitekelezea familia yake. Sisi watanzania wa leo vile vile tuamue tunataka Tanzania ya leo tu au ya Miaka zaidi ya 200 ijayo! Hivyo ndivyo walivyofanya wenzetu na kufikia hapa walipo. Maana mkiamua kuwa na Tanzania ya leo na kesho hamuwezi kukaa mnagombana juu ya udini,ukabila na ukanda,wakati hata watoto wengi bado wanakaa chini madarasani na kutopata milo mitatu. Itawabidi muwe kina BABA, mfikiri sana na kuamua yale yaliyo muhimu sana,muhimu kidogo na ya kipuuzi, na hapo mtakubaliana kuwa kwenye mambo ya msingi hakutakuwa na utofauti kwenye maamuzi. Sasa inapofikia Baba anaamua kumuchisha mtoto shule kisa mke wake hakumfulia nguo au kwa sababu anashangilia timu tofauti, maana yake ushabiki wa Simba na Yanga, Kufua nguo na Kusomesha vyote vina uzito sawa, sijui kama kunakuendelea hapo!
Vurugu tu za kiujenzi maeneo ya stendi kuu-Koln |
Tanzania ya miaka mingi mbele, inahitaji kuheshimu ukweli na kuweka uongo kando, inahitaji kutorudia makosa na kusamehe yaliyopita, inahitaji kuachana na visasi, inahitaji kufanya KAZI kwanza kuliko kitu chochote, inahitaji KUACHA UBISHOO/ inahitaji KUBANA MATUMIZI na kuwajibika na zaidi inahitaji kushirikiana kwa dhati, bila kujali itikadi zetu kwenye mambo yote ya kitaifa. HAYA YOTE YANAHITAJI KUCHEMSHA BONGO,HIVYO TUHESHIMU AKILI ZETU NA WATAALAMU WETU SANA. WATU WAZIMA HUFANYA MAAMUZI KUTOKANA NA AKILI NA SIO MISUKUMO YA NAFSI ZAO KAMA VIJANA, NDIO HASA WATANZANIA TUNATAKIWA KUWA HIVYO. Umefika wakati tujue kuna mambo ambayo hayapaswi kuamuliwa kwa kufuata chama,dini,kabila,rangi au utofauti wetu.Mambo kama afya bora,chakula bora,makazi bora, ajira na ujira,elimu bora,miundo mbinu bora na utaifa ni vitu ambavyo lazima ukweli uwe ukweli na uongo uwe uongo! UTAALAMU UWE MBELE KWENYE HAYO MAMBO, na sauti ya kila mtanzania juu ya hayo iwe moja kwanza ndipo tuendele kwenye michakato mingine. Na hata kunapotokea mabadiliko ya uongozi,mambo ya msingi yasibadilishwe na mtu au kikundi cha watu,bali na Watanzania kupitia wataalamu wao teule!
Carnevale- Siku Tano "kula bata" Babu zao waliumia na wao Wanalijua hilo na kuliheshimu, |
SWALIU LA KIZUSHI! We mipango yako sio ya kiujanjaujanja?
0 comments:
Post a Comment