Sunday, August 24, 2014

UJIFUNZE KUWA MTU, SIO MTU BORA KITU



1
Sisemi  usithubutu, Na mimi hula vya watu.
Ukiwa mtu wa watu, Uwe pia wao mtu.

Wasio gusa vya watu, Rohoni hawana utu.
UJIFUNZE KUWA MTU, SIO MTU BORA KITU.
2
Uwe makini we mtu, Wengineo sio watu.
Usoni tu ndio watu, Rohoni  mwao ni Chatu.
Wawe kwako ukurutu, Acha lao bulungutu.
UJIFUNZE KUWA MTU, SIO MTU BORA KITU.
3
Heri hata chuma kutu, Kifaacho wengi watu.
Kwao wewe sio kitu, Bora ya chao kiatu.
Nasema usithubutu, Kula vyao hao watu.
UJIFUNZE KUWA MTU, SIO MTU BORA KITU.
4
Na tena usithubutu, Kuwatoa wao utu.
Utamu wa kuwa mtu, Uyafanye yenye  UTU.
Uwe mtu mwenye utu, Si  mtu usiye utu.
UJIFUNZE KUWA MTU, SIO MTU BORA KITU.
5
Jifunze ishi na Watu, Wakuvalishe viatu.
Ujanani fanya utu, Uzeeni uwe mtu.
Ujanani Acha Utu, Ufariki kama jitu.
UJIFUNZE KUWA MTU, SIO MTU BORA KITU.
6
Binadamu ndio watu, na wengine sio watu.
Ibadani wapo watu, huwepo pia mijitu
Viongozi wapo watu, Wapo akili fyatu
UJIFUNZE KUWA MTU, SIO MTU BORA KITU
7
Wa timamu wapo watu, Punguani nao watu.
Wazee si wote watu, Vijana si wote watu.
Watoto wengi watu, japo tupo na tujitu.
UJIFUNZE KUWA MTU, SIO MTU BORA KITU
8
Sura yake hasa mtu,Ni tabasamu la utu.
Roho yake hasa mtu, Upendo matendo utu.
Fikira za hasa mtu,  Zatufaa  na mijitu.
UJIFUNZE KUWA MTU, SIO MTU BORA KITU
9
Maneno ya hasa mtu, Hayawakinai watu.
Tumbo la hasa mtu, Labakishia kajitu.
Elimu ya hasa mtu, Yawafaa  wote watu.
UJIFUNZE KUWA MTU, SIO MTU BORA KITU
10
Uwe wa kiasi mtu, Leo wengi sio watu
Usimuamini mtu, Pengine kameza Chatu.
Utu umekwisha kwetu, kwao ulikwisha utu.
UJIFUNZE KUWA MTU, SIO MTU BORA KITU

0 comments:

Post a Comment