Monday, July 22, 2013

SONGEA

Inauma kusikia, Songea imeumia.
SONGEA: Mwaka 1991, Yusuph Mayanga, Juma Ahmed Mpangule na Hamidu Abdalah

Nimekumbuka Songea, nimeshindwa vumilia.
Mfaranyaki tokea, majimaji tembelea.
Bombambili pandishia, Matarawe potelea
Inauma kusikia, Songea imeumia.

Manzese naijua, hasa niliposomea.
Lizaboni sikia, gundua uko Songea.
Misufini fikia, Majengo wakaribia.
Inauma kusikia, Songea imeumia.

Tuition fakamia, Walimu wako mamia.
Bei bure nakwambia, na Dar tulikimbia.
Hakika najivunia, masomo yao sawia
Inauma kusikia, Songea imeumia.

Siyo Mengi nayojua, machache nasimulia
Mjini ukisia, Kiswele imengia .
Taxi fukuzia, land rover kama mia.
Inauma kusikia, Songea imeumia.

Simba nayo Yanga pia, Magoli walibugia
Majimaji twatambia,vikombe yatuletea.
Viwanja vya kuchezea, ujuzi kujipatia.
Inauma kusikia, Songea imeumia.


Kigo ukiisikia, Boyz wamevamia
Kandanda walilijua,Umiseta wao mia
Girls Ruvuma pia, Zimanimoto sawia
Inauma kusikia, Songea imeumia.

Ngoma zilizotulia, dogori Lizombe pia.
Vyakula we fakamia,Wali,Ugali Bamia.
Vimwana sitoongea, Toto za kitanzania.
Inauma kusikia, Songea imeumia.

Si hata miaka mia,kasi iliendelea
Maendeleo mamia, mungu alitushushia.
Madini furumia, madigara kila njia.
Inauma kusikia, Songea imeumia.

Nakumbuka naumia, mji nilipendelea.
Mengi ya kuyarejea, ya mji ya kutetea
Nawaza na kuwazua, nini nitaufanyia.
Inauma kusikia, Songea imeumia.

He! Sasa ninasikia, Songea ni Tanzania.
Afadhali kukimbia,wengi wanapotea.
Magonjwa yamevamia, ya kama kwenye dunia
Inauma kusikia, Songea imeumia.

Majimaji  inalia, nani wa kuinyakua.
Viwanja tulochezea, mahindi wahifadhia
Siasa imevamia,Chabuluma wanalia. 
Inauma kusikia, Songea imeumia.


Mdachi Kombo sikia, Kilio nakutumia.
Vipaji ulivumbua, Amani Simba ajua.
Juhudi ulotumia, Liverpool wangeijua.
 Inauma kusikia, Songea imeumia.

Rafiki mwanisikia, Ni wengi kuwafikia.
Adam, Azizi pia, Chawanda, "Manu" sikia.
Mwnaharusi,"Kwio" pia,Wiliada  Teddy mia.
 Inauma kusikia, Songea imeumia. 

Walimu mimi nalia, Upendo najionea.
Haule, na Mango pia,Tawete na Ngoi mia
Viboko,Elimu nia, Nani leo anotambua
 Inauma kusikia, Songea imeumia.

 Napenda mimi kujua, Yepi yamewatokea.

Peramiho nako Pia,Kusini iliponea.
Nini kimetokea, Leo kutoisikia
Inauma kusikia, Songea Imeumia
 

Ni mengi ya kuongea, Na mengi ya kusifia.
Songea kweli Tambua,Uzima nakuombea.
Muumba akijalia, Hodi  hutaisikia.
  Inauma kusikia, Songea imeumia.  

Naomba wa kunambia, Si kweli ninosikia?
Songea yadidimia, vumbi lawatimkia.
Useme sababu pia, Songea ni Tanzania
 Inauma kusikia, Songea imeumia.

0 comments:

Post a Comment