Friday, August 9, 2013

SALAMU ZA IDDI - 2013!!!!!!



Thelatha kumi timia, Wetu mfungo sawia.
Mwana IDI katujia, Kheri katuletea.
Kesho tunafungulia, Ya kheri kutoachia
Salamu zangu pokea,Za  IDD nawatumia


Idi imetuwadia, Vema kusherehekea.
Kwa tende kufungulia, Kuswali kufuatia.
Chakula na familia, Vizuri kuzingatia
Salamu zangu pokea,Za  IDD nawatumia

Yake mola zingatia, Idi isije potea.
Sadaka ukishatoa , Acha tena kuwazia.
Njia uliyo ijia, Si vema ukarudia.
Salamu zangu pokea,Za  IDD nawatumia

Mengi mnayajua, Kafunza na BADI pia.
Muhimu kuzingatia, Ndio zangu njozi pia.
Imani bila ya nia, Matendo huwezi tia.
Salamu zangu pokea,Za  IDD nawatumia

Sita zitafuatia, Tufunge kwa dhati pia
Moja kutoiachia, Tuiweke yetu nia.
Mengi utayasikia, Yasije kutoa nia.
Salamu zangu pokea,Za  IDD nawatumia

 Rafiki zangu mamia, Fesibuku Twita pia.
Salamu nawatumia, Pongezi nawapa pia.
Heshima mliyoitoa, Iddi isije ishia.
Salamu zangu pokea,Za  IDD nawatumia

Napenda kuendelea, Mazuri kuyagusia.
Elimu niloishia, Zaidi nitakosea.
Kidogo niloongea, Samehe bila chukia
Salamu zangu pokea,Za  IDD nawatumia

Dua bora kumalizia, Hilo kubwa langu pia.
Ombi rohoni tokea, Muumba wetu sikia.
Tuongoze kwenye njia, Wako waso wako pia.
Salamu zangu pokea,Za  IDD nawatumia

0 comments:

Post a Comment