Sunday, July 21, 2013

SWAIBA KAMATA NJIA


“Swaiba kamata njia, Mimi nakusubiria”
Kama ndoto nakwambia, Siku hii kuwadia
Nauli imetimia, Sasa tuache kulia.
Hebu tiketi chukua, Nini wasubiria
Swaiba kamata njia, Mimi nakusubiria.


Machozi mbali futia, Safari sasa ngojea.
Punguza na kuongea, Mizigoyo fikiria.
Jioni ikiwadia, Siku imekukimbia.
Swaiba kamata njia, Mimi nakusubiria.

Zawadi kuniletea, Lazima nakuambia.
Useme nakutania,Haki nitakupasua.
Ukifika utalia, Huruma utanionea.
Swaiba kamata njia, Mimi nakusubiria.

TENDE mapema pakia, Zawadi ilotulia.
Peni Miswaki chukua, Ni muhimu kwako pia.
Sipendi kujipodoa, Leso na shuka chukua.
 Swaiba kamata njia, Mimi nakusubiria.

Usisahau bamia, Napenda kupindukia
Mchele pia Dagaa , Hata za Zenji chukua.
Unga wa lishe chukua, Wa uji kukorogea.
Swaiba kamata njia, Mimi nakusubiria.


Haya sasa naongea, Muhimu ya kwenye njia.
Ukweli nakuambia, Uwe makini na njia.
Achana na kudhania, Uwe macho mara mia.
Swaiba kamata njia, Mimi nakusubiria.

Kawaida twaijua, Mengi  utafikiria.
Hiyo haki yangu pia, Kuomba kutotokea.
Ya heri kwetu sawia, Si ya jela potelea.
Swaiba kamata njia, Mimi nakusubiria.

Hebu wewe fikiria, Ni wapi yanapitia.
Wenye ujanja mamia, Nini wanasafiria.
Usije kushtukia, Sumu imekuingia.
Swaiba kamata njia, Mimi nakusubiria.

Kupenda kusalimia,Viganjani angalia .
Hapo pata kutambua, Shaka si kwa kuongea.
Wengi tu maharamia, Kwa Mungu tutaungua.
Swaiba kamata njia, Mimi nakusubiria.

Usoni tumetulia, Waume na wake pia.
Marashi twapulizia, tupate watu vutia.
Uchafu tumeng’alia, Muumba twamchefua.
Swaiba kamata njia, Mimi nakusubiria.


Na mengi ya kukwambia, Vema nikisubiria.
Uwe makini na njia, Watu hatujatulia.
Si bajaji tu sikia, Nako Aiport pia.
Swaiba kamata njia, Mimi nakusubiria.

Aga ndugu na jamaa, Usiteme zao dua.
Wana mengi usojua, Ya akhera ya dunia
Mboni zao kama Jua, Kote zitakufikia.
Swaiba kamata njia, Mimi nakusubiria.

Beti kumi nina nia, Radhi utajaniwia.
La mwisho sijaongea, Hebu acha kusinzia.
Kuwepo  kwenye mkia, Si Uzito bali Nia.
Swaiba kamata njia, Mimi nakusubiria.

Kicheko nakihisia, Chozi lakulenga pia.
Pendo bora ndio nia, Muumba akijalia.
Kila siku Ombea, Pendo aje lizindua.
Swaiba kamata njia, Mimi nakusubiria.

Mwelevu atang’amua, Shairi tajifunzia.
Nomino  atatupia, Swaiba tamwimbia.
Wapo na wenye kunoa, Shairi watapondea
Swaiba kamata njia, Mimi nakusubiria.




0 comments:

Post a Comment