Wednesday, July 17, 2013

Mchumi wetu Mchumi, Mchumi acha umimi



Mchumi huyu Mchumi, Mchumi wetu mmimi.
Apanga mambo kivumi, Apangavyo si kichumi.
Kupanga huku uchumi, Kupanga gani Mchumi.
Mchumi wetu Mchumi, Mchumi acha umimi


Kwako posho mara kumi, Senti humo simo  mimi.
Hapo waleta umimi, Wafanya sivyo Mchumi.
Humjali wa Mikumi, Wamjali wako Vumi.
Mchumi wetu Mchumi, Mchumi acha umimi

Asiye na hela kumi, Apata hewa mchumi.
Haendi juu ya lami, Hapandi ndege mchumi.
Usibishe we mchumi, Usije pigwa na ngumi.
Mchumi wetu Mchumi, Mchumi acha umimi

Tatizo lako Mchumi, Hupendi acha umimi.
Hulali Tanga na mimi, Msiba dili kichumi.
Ukianguka  uchumi, Niwe Mkombozi mimi.
Mchumi wetu Mchumi, Mchumi acha umimi


Na nyie akina mimi, Msiwe kama mchumi.
Nyumbani mko na mimi, Jumbani wenu mchumi.
Maandamano na mimi, Magawano na mchumi.
Mchumi wetu Mchumi, Mchumi acha umimi

Mnampenda mchumi, Mnanitenga na mimi.
Asilimia  ya kumi, Asali  mia mchumi.
Mwala mbuzi wa uchumi,Mie nyama ya ulimi
Mchumi wetu Mchumi, Mchumi acha umimi

Kila alipo Mchumi, Hataki niwepo mimi.
Kila mzigo mchumi, Ataka nibebe mimi.
Kila mtu ni mchumi, Umo utemi na ngumi.
Mchumi wetu Mchumi, Mchumi acha umimi

Kila jambo la mchumi,Kila chaguzi mchumi.
Kila nafasi Mchumi, Kila safari Mchumi.
Kila andiko Mchumi, Kila jadala Mchumi.
Mchumi wetu Mchumi, Mchumi acha umimi

 Uchumi tule na mimi, Unifunze na uchumi.
Yangu nipange mimi, Yetu tupange na mimi.
Yangu nile sana mimi, Nisikutupe mchumi
Mchumi wetu Mchumi, Mchumi acha umimi

Uchumi sio Umimi, Ona wenzio Wachumi.
Vijana wao makumi, Wanamiliki uchumi.
Hawakusoma Miami, Kenya wapo Wachumi
Mchumi wetu Mchumi, Mchumi acha umimi






0 comments:

Post a Comment