Saturday, August 17, 2013

ZAMANI KUNA MBELENI

1

Enyi wetu wa zamani,Radhi yenu niwieni.
Wekeni yenu pembeni,Someni yangu hewani.
Mimi sio wa zamani,Napenda jua zamani.
Yangu haki naamini,Yangu kuweka hewani.
Kwa wote mlo makini,Yawekeni  akilini.
Yeyote mwenye imani, Msingi wake zamani.
TUMEITUPA ZAMANI, TUTAJUAJE MBELENI.

2
Ukisahau zamani,Umesahau mbeleni.
Wale walio mbeleni,Wali ijali zamani.
Mazuri yao zamani,Tuyafanye zetu mboni.
Mabaya yao zamani,Tusiyatupe chooni.
Tuyaweke vitabuni,Wajifunze wa mbeleni.
Yasiishie darasani,Yabobee mitaani.
TUMEITUPA ZAMANI, TUTAJUAJE MBELENI.

3
Mijini na vijijini,Kote kwetu jamani.
Ni wapi hasa mjini,Hapakuwa kijijini.
Sisemi toka mjini,Sisemi nenda mjini.
Ukijua muda nini,Hoja iko akilini.
Mijini Vijijini,Muhimu ni una nini.
Wangapi tupo mijini,Mizizi si vijijini?
TUMEITUPA ZAMANI,TUTAJUAJE MBELENI.

4
Ukiitaka amani,Waheshimu wa zamani.
Wanayo mengi madini,Yatufaayo mbeleni.
Hebu acheni utani,Nafsi sio Madini.
Tumeanza kiutani,Kuidharau zamani.
Tutaisaka amani,Ng’ambo nako milimani.
Kurudi  tutatamani,Kusaka hii amani.
TUMEITUPA ZAMANI,TUTAJUAJE MBELENI.

5
Jamani yetu zamani,Jamani tuithamini.
Kwa akili jadilini,Na uwingi umakini.
Mtoe yetu maoni,Ya mwenu hasa vichwani.
Roho zetu hatarini,Hili liwe fikirani.
Ujinga tunathamini,Walio juu na chini.
Akili zetu udini,Afya, chakula cha nini.
TUMEITUPA ZAMANI, TUTAJUAJE MBELENI.

6
Elimu iko sokoni,Elimu sasa vimini.
Mkubwa aseme nini,Mkubwa kawa wa chini.
Kufoka afoke nani,Kufoka afoke nini.
Vitabu tena vya nini,Kila kitu kiganjani.
Kusoma sana kwa nini,Kusoma faida nini.
Muda wote vijiweni,Ubishini ni kazini
TUMEITUPA ZAMANI, TUTAJUAJE MBELENI.

7
Mamia mamilioni,Hoja zetu ni laini.
Zikitufaa  machoni,Si muhimu akilini.
Tazama mitandaoni,Hakika  utabaini.
Asubuhi na jioni,Tuna hoja milioni.
Kwa makini tathimini,Thamanize huoni.
Kadhaa zenye thamani,Azisomae ni nani?
TUMEITUPA ZAMANI,TUTAJUAJE MBELENI.

8
Mazuri tujadilini,Yajae na akilini.
Ya kijinga yaacheni,Yafie mwangu kichwani.
Hapo na tutabaini,Tekinolojia nini.
Wazee wetu zamani,Walijua vya thamani.
Akili walithamini,Waliacha ya moyoni.
Tuwajibike jamani,Ndio msingi makini.
TUMEITUPA ZAMANI,TUTAJUAJE MBELENI.

9
Ni nani hasa ni nani,Ambaye yuko makini.
Aturudishe zamani,Atuongoze mbeleni.
Awe hasa ukwelini,Atufaye masikini.
Nawaona wa zamani,Si muoni wa mbeleni.
Najihisi ni motoni,Bora iwe ni ndotoni.
Subiri serikalini,Subiri mpaka lini?
TUMEITUPA ZAMANI, TUTAJUAJE MBELENI.

10
Nina mengi ya kughani,Wachache watabaini.
Ubovu wa fikirani,Wameishia njiani,
Hawatasoma ya chini,Ya juu welevu chini.
Hawasomi yalo chini,Hawawahi Kanisani.
Sio wa Misikitini,Sio waenda kazini.
Wao lengo si maoni,Ulumbani milioni.
TUMEITUPA ZAMANI, TUTAJUAJE MBELENI.

11
Tazama yangu zamani,Jiulize kuna nini.
Hesabu sio makini,Hata unifanye nini.
Huniwezi uwanjani,Huniwezi hasilani.
Wa hesabu themanini,Uwanjani sifurini.
Amina bingwa jikoni,Amiri bingwa kwayani.
Tukifanya mitihani,Sifuri ni yake nani.
TUMEITUPA ZAMANI,TUTAJUAJE MBELENI.

12
Kwetu ni Uswahilini, Sio huku ushenzini.
Maisha Bora Mbugani, Sio jilunda Mjini.
Tiba Hospitalini, Sio fia Marekani.
Tunairuka zamani,Tudondokee  puani.
Tuharibike vichwani,Tumeguke na nyongani.
Tunapenda mitihani,Tunapenda ya vyetini.
TUMEITUPA ZAMANI, TUTAJUAJE MBELENI.

13
Hebu mniambieni, Wapi kwetu viwandani.
Waulize wa zamani, Toka kote mikoani.
Walienda viwandani, Wengine maofisini
Kidogo cha mfukoni, Kiliwafaa nyumbani.
Elimu bure shuleni, Usafiri hadi Relini.
Leo Ujinga vichwani,Mabenzi barabarani, 
TUMEITUPA ZAMANI, TUTAJUAJE MBELENI.

14
Hayatufai jamani,Hayafai asilani.
Tukikumbuka zamani,Tumetoka sifurini.
Tujali yetu zamani,Tuwe bora fikirani.
Watanzania jamani,Ukweli sasa semeni.
Amani i hatarini,Ubovu u fikirani.
Serikali hasa nini,Si tutoke sifurini.
TUMEITUPA ZAMANI, TUTAJUAJE MBELENI.

15

Viongozi wa zamani,Tuliwapata zamani.

Hapana nyie bisheni,Imani yangu acheni.

Busara fikirani,Akilini umakini.

Uongozi una Dini,Daudi na Selemani.

Hakika utabaini,Uongozi sifa nini.

Kisha mtafakarini,Kura zatufaa nini.

TUMEITUPA ZAMANI, TUTAJUAJE MBELENI.


16


Mipango mingi Bungeni, Kumi asilimiani.

Wakuu wengi nchini, Masilahiyo mbonini.

Reli zetu za zamani, Anayeziua nani?

Vipaji vyetu makini, kavitelekeza nani?

Kiswahili chetu Dini, Asiyejali ni nani?

Mti fisadi nchini, Aliyeupanda nani?
TUMEITUPA ZAMANI, TUTAJUAJE MBELENI. 

17


Hebu zama  kimakini, Ujue tatizo nini
Walio serikalini, Elimu wao Tisini.
Mengi yetu ya zamani, Wanayasifu surani.
Wayasema jukwaani, Yanawabeba kurani.
Wajapo tu vitendoni, Wameyatupa Kapuni.
Mboni mwao nafsini, Yetu kesho kwao nini?

TUMEITUPA ZAMANI, TUTAJUAJE MBELENI.

18
Ubora tu fikirani,Jibu lililo makini.
Serikali isemeni,Serikali i pembeni.
Iwaone hasirani,Iwakute vitendoni.
Tutokeni siasani, tujikite kilimoni.
Tukiitwa jukwaani, tuwaite mashambani
Wakaribishe nyumbani, Sio  mwetu mifukoni
TUMEITUPA ZAMANI,TUTAJUAJE MBELENI.

19


Uzeeni ujanani, Ujanani uzeeni.
Umakini duniani,Ujanani Uzeeni.
Utusi kwenu nyumbani, Ujikute jalalani.
Ujinga wa ujanani, Utoto wa uzeeni.
Ubora wa Uzeeni, Ubora kesho nyumbani.
Ubinafsi nyumbani, Utumwa wetu mbeleni.
TUMEITUPA ZAMANI,TUTAJUAJE MBELENI
 
20
Ninamuomba manani,Afumbue zetu Mboni.
Tuelewe ya zamani, Yatufae kwa mbeleni.
Yasitutie vitani, Yatutoe sifurini.
Tuwapate makuhani, Kama Musa na Haruni.
Wasije mahayawani, Wenye nuko nafsini.
Tuboreke fikirani, Tuone chele pumbani
TUMEITUPA ZAMANI,TUTAJUAJE MBELENI

2 comments:

  1. Ama kweli ZaMaNi inapendeza Zamani hata mapenzi yalikuwa zamani, kuwajibika zamani kwa kila mwenye shughuli yake, malezi yalikuwa zamani baba aliwajibika na mama pia, thamani ya kila mtu ndugu jamaa marafiki jirani nk ilikuwa zamani hata thamani ya mpangaji kwa mwenye nyumba ilikuwa zamani.
    nimeipenda na kupenda mengi ya zamani.
    Asante sana bro.

    ReplyDelete
    Replies
    1. Nashukuru sana! Usiitupe zamani,Yako uipe thamani. Uifanyie ya ndani, ikuongoze mbeleni.

      Delete