Sunday, March 23, 2014

Uchama si ufitini, Ukabila si udini



1
Sasa mimi naamua,Maji nguo navulia.
Sifuri ukiijua, Utaandika na mia.
Bora kiguru na njia,Tuli bure huumia.

Kufika ukikawia, Pata ulichofikia.
Sikia ya kusikia,Maanaze dadavua.
Upande wako dandia,Undaniwe pambanua
Uchama si ufitini, Ukabila si udini
2
Kimbia ama tembea, Linganisho fikiria.
Matamu yao Ongea, Hakikisha wayajua.
Bweteka sio tulia, Hutakosha sufuria.
Kesha mvua na jua, Ya muumba fikiria.
Panga hata kwa jambia, Ya muhimu zingatia.
Mwenye kweli yenye nia, Nyendoze huwa sawia
Uchama si ufitini, Ukabila si udini
3
Yavuma kupindukia, Pasuka utasikia.
Katu usije kimbia, Tukioni sogelea.
Ngoma ikishatulia, Mizuka itapungua.
Kelele zitapungua, Hasara tutaijua.
Ujinga utapotea, Welevu tutaujua.
Umoja utajongea, Hesabu zitatukaa .
Uchama si ufitini, Ukabila si udini
4
Kushoto ama kulia, Hakuna kulotulia.
Zamani kushikilia, Ujinga ulotulia.
Ujinga kuurukia, Uchizi wa kudhania.
Dini kupuuzia, Sayansi kutoijua.
Kabila kuinamia, Gizani kutokomea.
Akili ukitumia, Ya moyo utapembua.
Uchama si ufitini, Ukabila si udini
5
Sifuri ukiijua, Muhimu utagundua.
Uchama wetu pembua, Viini vimeungua.
Udini wetu chungua, Uungu hutoujua.
Ukabila sio pua, Hatukosi kupumua.
Ukweli sasa gundua, Sifuri kutoijua.
Welevu wameng’amua, Wapi pa Kututungua.
Uchama si ufitini, Ukabila si udini
6
Napenda sana ongea, Machache ninayojua.
Kusoma bado kujua,Ubovu yangu tabia.
Sifuri yangu fichua, Fikira ziwe sawia.
Uchama ningechagua,Fitina wapi kwepea.
Kabila sito kimbia, Ukabila napembua.
Udini wangu wa poa, Mbinguni nime potea
Uchama si ufitini, Ukabila si udini
7
Fikiria dadavua, Kosoa nilokosea.
Sifuri yako chagua, Vema nami nikijua.
Tanzania yaungua, Huamini we funua.
Uchama wafurumia, Ujinga kushabikia.
Udini unachanua, Hakuna wa kuzuia.
Ukabila tunafufua, Ujinga umekolea.
Uchama si ufitini, Ukabila si udini





0 comments:

Post a Comment