Maamuzi ni vema Yakazingatia vizuri WAKATI WETU.
Kama nimeelewa hoja, ni kuwa kwa kuwapunguza wachezaji wa kigeni walau kwa asilimia walau 50, kuna uwezekano tukaongeza nafasi ya wachezaji wa nyumbani kupata nafasi katika timu zao za kwanza za vilabu vyetu. Na kimsingi kwa kama hilo litatokea kuwa hivyo matarajio ni kuwa
1. Wachezaji
watapata kucheza mechi nyingi na zenye ushidani za kutosha kuongeza uimara wa
kuweza kutupatia matokeo mazuri zaidi katika timu yetu ya taifa.
2. Vilabu
vya Tanzania kuthamini wachezaji wa umri mdogo AMBAO NI WAZAWA na ikiwezekana kuwaandaa wenyewe kupitia timu zao
za watoto wadogo kama sio kuziimarisha kabisa hizo timu.
Hili linaweza kuwa sahihi, KWA UPANDE FULANI. Yaani, ukichukulia kuwa timu
kama Simba, Azam au Yanga, zina
mchango mkubwa katika timu ya Taifa, kwa
kutoa wachezaji wengi na pengine kwa maendeleo ya mpira nchini. Pamoja na
kuwa na timu za vijana,bado mara nyingi
kipaumbele ni mafanikio yao katika mashindano makubwa, na hivyo uhitaji
wa wachezaji wenye uzoefu na uwezo mkubwa ni chaguo lao zaidi ya wachezaji
wachanga.Kwa hiyo, Moja ya sababu ya kupenda kusajili wachezaji wa kigeni,
ambao wanaamini na kwa hivi karibuni wamekuwa wakisaidia kufanya vizuri kwa
timu hizo, inaweza kuwa ni TAHADHARI YA
KUPATA HASARA YA KIPESA kwa kutumia pesa nyingi kuandaa hao vijana wakati
nafasi ya hao vijana kufanya vema kwa haraka kwenye mashindano makubwa ni
ndogo. Kwa hiyo inakuwa ni hasara kwao.
Kama hoja ni hiyo, naamini pia mtazamo unachukulia kuwa:
1.
Timu nyingi
za Ligi Kuu, hasa zile zenye mchango mkubwa wa wachezaji katika timu ya TAIFA, zinatumia
wachezaji wa nje kwa kiwango kikubwa katika mechi zao za ligi na zina uwezo wa
kuchukua wachezaji walau hadi 10, kama
sheria inavyowataka kwa sasa.
2.
Idadi
inayopunguzwa ya wachezaji wa kigeni, haitapelekea kuharibika kwa mafanikio ya
kibiashara ya timu na kusababisha timu hizo kushindwa kwenda kwenye hatua kubwa
za mashindano amabzo ndio muhimu kwa ubora wa wachezaji wa nyumbani
3.
Mazingira
mengine ya uendeshaji wa mpira kama vile timu za watoto wadogo na malipo ya
wachezaji wa aina zote ni mazuri kwa kila timu.
4.
Na
pengine, mchezo wa mpira wa miguu kwetu umefikia hatua nzuri ya Kitaalamu. Hivyo
wachezaji wakipewa nafasi watatumikia vema na waajiri au vilabu viko tayari
kulipa stahiki zao bila shida.
Kuna watu wanaamini kuwa hii sio njia sahihi, ukisoma maandiko katika
mitandao, watu kadhaa kutoka Tanzania, akiwemo Haji Manara (Mkuu wa Idara Ya Habari Na Mawasiliano
ya Klabu Bingwa Tanzania Bara na mabingwa wa kihistoria kwa mechi za kimataifa
nchini Tanzania, mtoto wa mmoja wa mastaa wakubwa katika historia ya mpira wa
miguu nchini Tanzania, Haji Sunday Manara-http://www.dar24.com/haji-manara-apinga-kupunguza-wachezaji-wa-kigeni/). Kwao njia sahihi ingekuwa kuboresha VITUO VYA
WATOTO wadogo na kuweza kuandaa vipaji vyetu ili vijana waweze KUIVA KITAALAMU
katika mchezo huu. Kwao, pengine kupunguza wachezaji hukuondoi mzizi wa tatizo,
kwa sababu hata idadi ya wachezaji wa
nje sio kubwa kiasi cha kusema kinaathiri ubora wa timu ya taifa. Na pengine
kufanya hivyo kutapunguza zaidi nafasi ya timu kubwa chache zenye wachezaji hao
wa kigeni wengi, za nchini kuweza kushindana kimataifa na hivyo kushusha
mafanikio yao kibiashara pia.
Ukisoma https://ghanasoccernet.com/egyptian-fa-to-reduce-foreign-players-quota, unaweza kuona jinsi swala hili
linavyochukuliwa na mashabiki wa soka baada ya Misri kupunguza idadi kutoka wachezaji
watano mpaka wanne wa kigeni.
Ulaya pia swala linaloendana na hili limewahi jadiliwa mara kadhaa. Ukisoma
kwenye maandiko kama lile la (Smokvina, 2013) kuhusu taratibu za
idadi za wachezaji wenyeji na wageni, na hata wale walio chini ya miaka 21,
bado inaonekana lengo hasa la taratibu za namna hii, ni kujaribu kuweka usawa
kati ya biashara za timu husika na manufaa ya nchi. Japo kuna hoja kadhaa za
kuashiria kuwa matokeo ya mipango hii bado haijatoa mafanikio ya kuridhisha
kuweza kusema ni taratibu sahihi kwa malengo yake. Wengine wanaamini ni mifumo
wenye mapungufu ya kisheria pia. Yaani, uhuru wa wachezaji kutoka kutoka nchi
moja hadi nyingine ni kama unaingiliwa pia kwa kiasi fulani.
Changamoto kubwa ninazoiona ni kupata uwiano sahihi wa maslahi. Wote
tunataka mafanikio ya nchi katika soka, lakini tofauti ni njia gani ni sahihi
kuyafikia mafanikio hayo. Mimi kama shabiki, ninachotaka ni furaha ya kila siku
mpaka nakufa. Kama mteja namba moja ninachohitaji ni kuona timu yangu ni bora
kuliko zote ulimwenguni. Na upande mwingine, kama mzalendo na mwenye kuhitaji
maendeleo ya kitaifa, napenda kuona mtanzania anapewa kipaumbele kwanza, ili
pesa yangu ijenge nchi yangu pia. Swala la kuandaa vijana au wachezaji
wa taifa, nitapenda lifanyike lakini lisizuie uwezo wetu wa kimataifa kila
mwaka.
Binafsi naamini Simba, Yanga na zinginezo ni timu saidizi tu za
serikali katika kuandaa timu ya taifa au kuendeleza mchezo huu nchini.Serikali ina jukumu la kuweka
mazingira mazuri kwa wote ikiwemo timu kubwa katika kuhakikisha ndoto za timu,
mashabiki,wananchi na vijana machipukizi zinatimia. Baadhi ya raia Afrika ya
Kusini, waliwafukuza watanzania na watu wa mataifa mengine wakiamini ndio
chanzo cha wao kukosa kazi na pengine maisha mazuri.Wanaweza kuwa sahihi,
lakini siamini kama huo ulikuwa mzizi wa maisha yao kuwa magumu au kuwa
hakukuwa na namna nyingine ya kulizuia hilo. Kupunguza maumivu ya kichwa
unapougua malaria ni jambo jema ili walau uweze kuendelea kuandika porojo
muhimu kama hizi, lakini kuondoa wadudu wa malaria hata kama ni kwa sindano, ni
muhimu sana ili kudumu katika hali nzuri kiafya dhidi ya malaria. Serikali isisite kuanza safari ya kuondoa wadudu wa malaria kwa sababu hakuna mwingine wa kusaidia katika hilo.
Kwenye michezo, wimbo wa tuwajali vijana na vijana taifa la kesho nimeusikia
miaka Zaidi ya thelathini sasa. Sio kwamba hakuna kinachofanyika, la hasha, ila
siamini kama kinachofanyika kinatosha. Pengine tunasubiri MUDA utulazimishe. Kuna
wengi wanafanya mengi mazuri, kwa jitihada binafsi hapa nchini naamini.Ila
siamini kama inatosha kwa mtu au taasisi binafsi kufanya jambo la kitaifa bila
nia na msaada madhubuti wa kimiundombinu kutoka serikalini. Namkumbuka mwalimu
wangu Mdachi Kombo, aliyekuwa mchezaji wa timu ya Majimaji. Alifanya
kazi kubwa sana pale Songea, kwa kuanzisha timu ya vijana wadogo, nikiwemo mimi
na mashindano ya timu za vijana na hadi viongozi wa Majimaji wakaburudika sana.
Vijana kama Masumbuko Makalisha na Amani Simba, walifanya vema Mtibwa na Simba,kwa
kiasi kikubwa maandalizi hayo yaliwasaidia. Swali ni wapi alipo Mdachi Kombo? Nini
kilimkuta akaacha kuzalisha wachezaji wengine? Na cha ajabu hao wachezaji
wawili sijui ni yupi aliwahi kuchezea Majimaji. Alichofanya Mdachi Kombo ni
kitu cha kujitolea, ambacho kimsingi atalipwa na MUNGU. Kimsingi kitu kama hiki
kilipaswa kupewa mazingira mazuri kumsaidia Mdachi Kombo ama kufanywa na
serikali ili kiwe cha kudumu.
Serikali inapaswa kujitolea Zaidi kwenye hili kuliko taasisi au mtu
mwingine.Wakati Napata habari kuwa Gharib Said Mohammed (GSM), anayehusishwa
na Dar Young African, mabingwa wa kihistoria wa kombe la Tanzania Bara, kuwa ni
kati ya wachezaji watimu ya watoto ya Liverpool ya Mdachi Kombo pale Songea,
nilifurahia sana mafanikio yake kifedha, ila nikaahidi kuwa nikipata nafasi ya
kuongea naye, nitamuuliza kwa nini hakuanzisha timu za vijana kama ambavyo Mdachi
Kombo alivyofanya.Nadhani Mo
Dewji, mdhamini wa timu niipendayo pia, aliliweka hili wazi kuwa
anahangaika na Simba kwa sababu kibiashara JINA la Simba linaweza kumpa uwiano
mzuri wa Maslahi kuliko kuanza chini.
Najivunia sana kuwa mmoja wa wanaMpaju FC (https://www.mpajusc.com/), naamini mzee Mdachi Kombo,atajivunia
pia kuona kijana wake angalau kafuata nyayo zake. Kama ningepewa nafasi ya
kushauri, nadhani ningesema yafuatayo:-
1.
Timu
yenye uwezo wa kusajili hata wachezaji Thelathini wa KIGENI, ipewe uhuru wa kufanya hivyo.
Muhimu ni kuangalia ni jinsi gani, taifa linaweza kupata thamani nzuri kutokana
na uwepo wa hao wachezaji. Leo hii akiwepo Messi katika timu
zetu nchini, radha ya mpira na hata biashara yake itapanda na kuleta mambo mengi
chanya katika nchi. Labda waingereza wao utaratibu huu unaweza
usiwafae kutokana na hatua waliyopo kimaendeleo. Lakini hata sisi huenda
tukifika hatua nyingine tutabadili muundo ili kwendana na wakati, ila kwa sasa
nadhani tunahitaji zaidi kuufanya mchezo uwe Elimu, Burudani,
Biashara,Ajira,Afya,Malezi na Furaha nchini, zaidi ya kufanya vizuri kimataifa kama taifa. Acha Simba na Yanga ziende na zifike popote zinapoweza kama timu.
2.
Jukumu
la mafanikio ya timu ya Taifa na vijana wenye vipaji ni jukumu la serikali. Hivyo serikali, iweke
na kusimamia sheria ya ligi za watoto. Hakuna sababu timu zote kupenda kuwa madaraja ya juu badala
ya kupenda mpira na mafanikio yake katika ngazi zote. Fikiria kama kila Kila kata au Wilaya iwe na ligi
kama ya Mpaju Cup http://mpaju.blogspot.com/2019/09/mpaju-cup-2019-yahitimishwa-na-kiongozi.html. Ligi kama hii inahitaji pesa kidogo tu
kuianzisha na baadae itajiendeleza yenyewe baada ya wazazi kuona na kufahamu
kuwa nayo ni sehemu ya elimu na malezi kwa vijana wao.
3.
Sijui kama mashindano ya kitaifa ya shule za sekondari na msingi ni ya muhimu sana kwa wakati tulionao. Naamini tunahitaji
taratibu,muda,maeneo na taasisi binafsi nyingi zinazojishughulisha na michezo
na sanaa kwa watoto na jamii yetu. Kama tunaweza kupambana na magonjwa, hakuna
tunachoshindwa kuweka na kusimamia mikakati ya michezo kwa ajili ya vijana.
Tuwe na vituo vya kujifunza muziki,mpira na kadhalika mitaani. Mashuleni
watoto wasome vyote kama masomo na viwanja vyao na maeneo yao yatumike kama
sehemu za majaribio na mazoezi au mashindano ya kirafiki. Sidhani kama
tunahitaji mashindano ya mashuleni na kuwakusanya vijana kwenye umiseta na
umishumta kama zamani. Wakati umepita wa kufanya hivyo. Tanzania House Of
Talents (THT) iko Dar Es Salaam tu, kwa nini? Viwanja vya JK viko Dar. Kila kitu ni DSM, kwa nini? Uwiano wa maslahi bado ni bora Dar....! Mbeya
hata kiwanja Ngoma kimekufa kabisa, mahali ambapo naambiwa wachezaji kama Sekilojo Chambua wanapafahamu pia.
4. Tuwafanye
watoto kuwa kiini katika dira yetu ya michezo, mengi yatafunguka ya leo na ya kesho. Najua wabeijingi
watauliza, kwa nini watoto na sio wao? Jibu la hilo swali kwangu mimi ni sijui. Sijui tumelogwa na nani? Angalia michezo ya vijana, si ajabu kuona
mpaka leo watoto mtaani wanacheza bila viatu. Sasa vipi kuhusu sheria za mpira au misingi ya
kitaalamu ya michezo wataijuaje?Tuanze leo na tuanze na Mpaju Sports Centre.
Kocha Ali Mkumbukwa Akiwa na Vijana wa U-12 Mpaju FC wakati wa Mapumziko uwanja wa FFU Mbeya |
Mpaju FC wakiwa kwenye Picha ya Pamoja wakati wa Tamasha la Mpaju Week 2019 Uwanja vya Magereza Mbeya |
Mpaju FC U-12 wakisubiri Kuchuana na Shule Msingi Mpolo Wasichana U-15 Uwanja wa Magereza Mbeya wakati wa Mpaju Week 2019 |
0 comments:
Post a Comment