Sunday, March 10, 2013

SHIRIKA LA NYUMBA LA TAIFA (NHC): MAISHA NI NYUMBA NA NYUMBA NI PESA!



 "KAMA TUSIPOPATA FAIDA IMEKULA KWA WALALAHOI MARA MBILI"

NANUKUU Taarifa iliyotolewa na Shirika la Nyumba, ya 24/10/2012 kwenye uzinduzi wa uuzwaji wa nyumba mradi wa MINDU,Dar Es Salaam, “Kila nyumba itauzwa kwa bei ya TZ S 272,050,673.08 bila kodi ya ongezeko la thamani (VAT ) na  TZS 321,019,794.24 ikiwa na  kodi ya ongezeko la thamani  ( VAT )

Tunawahamasisha na kuwakaribisha watanzania wote walio nchini na nje ya nchi kujitokeza ili kununua nyumba hizo. Wanaweza kufanya mawasiliano na Makao Makuu ya Shirika, Ofisi zetu za Mikoa au kupitia barua pepe na kukamilisha taratibu mapema kwa ajili ya kuweza kuingia kwenye mchakato ulio wazi wa manunuzi.

Katika kutekeleza miradi ya ujenzi wa nyumba, Shirika linajenga nyumba za gharama ya juu, kati na chini ili kuwahudumia watanzania wa kada zote. Katika azma hiyo, nyumba 10,000 zitakazojengwa kufikia 2015 zitahusu watu wa kipato cha juu na nyumba 5,000 zitakazojengwa kufikia mwaka huo zitakuwa ni nyumba za watu wa kipato cha chini.

Shirika limeanza kujenga nyumba za gharama ya kati na juu ili kupata faida itakayoliwezesha kuwajengea watu wa kipato cha chini nyumba za gharama nafuu. Hii inatokana na ukweli kuwa Shirika halipati ruzuku toka serikalini ya kujenga nyumba kwa ajili ya wananchi wa kipato cha chini”. 

Naipongeza Serikali kuongeza Juhudi za nyumba kupitia NHC. Na hata ujenzi wa barabara ambao kwa ujumla tumeushuhudia siku hizi za karibuni. Mengi naamini yanaendelea mazuri na yana wezekana.Labda cha kuongelea kidogo  katika kuboresha hili la nyumba ni;

  • Swala la rasilimali zinazotumika ni zaidi za Watanzania? Utaona kwenye eneo la utawala na uongozi kwa kweli kuna furahisha! Ni watanzania zaidi! Na hivyo naaminia kwenye maeneo mengine kama vile  wafanyakazi na Vifaa maofisini na hata kwenye maeneo ya ujenzi na ununuzi,vyote vitakuwa ni zaidi kutoka Tanzania.Sio kosa kuona nini kwanza tunaweza au kinatunufisha sisi kama watanzania kabla ya kuona wapi tuombe msaada bora! Na unapotumia vifaa vingi kutoka nje, nahisi kama unaweza kuwa unawanufaisha zaidi watu wa nje. Lakini maadamu tunapata nyumba bora, potelea mbali bwana.
  • Tukija  kwenye nyumba zenyewe, zinaendana vipi na malengo ya Taifa? Zile za Kigamboni Housing Estate zenye vyumba vitatu kwa ukubwa wa 70m² na vyumba viwili ikiwa na ukubwa wa 56m²,si dhani kama ni za mtanzania wa kipato cha chini. Asilimia kubwa ya watanzania hawataweza kumudu kununua nyumba ya shilingi 45,000,000/= ambayo ukikopa benki,utalipa sio chini ya Tshs 500,000/= kwa mwezi au 12,000,000/= .Pengine itamuhitaji mtanzania huyo kutumia miaka 25,kumaliza malipo. Japo atakuwa anafurahia nyumba yake, lakini, ili aipate anahitaji kipato cha walau 1,000,000 kwa mwezi, ili awe ametumia 50% ya kipato chake kujengea nyumba. Ngumu saana, na zaidi itakuwa ni kuandaa nyumba za watanzania wachache wataokuwa wanawapangisha wengi baadae! Na Kwa kweli ndio ilivyo duniani tunakoiga! Na kwa hiyo,tunaweza kukubaliana kuwa hakuna nyumba ya kima cha chini,hata zile 5000/= ni za kima cha kati.
  • Nyumba ni maisha ni mpango mzuri, ila uboreshwe kwa kuwa na upande maalumu wa kujenga nyumba za kitanzania kwa ajili ya kundi la kipato kidogo cha mtanzania! Soko lisiwafanya NHC wakatoka nje ya malengo ya kitaifa! Makazi yawanufaishe Walimu, madaktari wadogo ,manesi,wafanyabiashara wadogo hata kama vijijini na mapembezoni mwa miji watakuja tu! Tulisoma ili kuweza kuisaidia jamii kulingana na hali tuliyonayo na sio kwa kufikiri kama waliotufundisha jamani. Kuna maneno ya kitaalamu yametumika, KIUCHUMI/KIBIASHARA, kuwa tunaanza kuwaangalia walio juu na kati kwanza,ili tupate faida,itakayotusaidia kuwajengea wale wa kipato cha chini baada ya 2015.  Hivi, hapa ndio kufikiri kwetu kulipofikia? Na kweli kabisa kwa mazingira ya Kibongo, tutarudi kuja kumwambia huyu mtanzania wa kipato chini kuwa hii ndio faida sasa ngoja tukujengee? Au ndio zitaibuka hadithi zingine? Pesa bwana haishi mahitaji, tukimaliza kujenga hizi,tutagundua kuwa tunahitaji kumalizia na shule za wenye pesa kwanza,ili tupate faida safi itakayotuwezesha kumjengea masikini nyumba ya kisasa zaidi,na baadae tutagundua kuwa ni heli,tuanze kwa kujenga hospitali ilimasikini huyu akiugua atibiwe,na mwisho ……! NA TUSIPOPATA FAIDA, TUJUE IMEKULA KWETU MARA MBILI.
Mtazamo wa Tanki katika hili!
1)    Tunategemea, wataalamu wameona kuwa ni muhimu kuanza na matajiri kwanza, hivyo tungeomba wanauchumi na wataalamu wa biashara kutuhakikishia hilo kuwa ndio sahihi. Lakini, kwa FIKRA za tankini, makazi bora ni haki ya Mtanzania, kama tunahitaji kumsaidia,basi tuangalie kutokea kwenye rasilimali alizonazo,na sio mitazamo yetu ya miaka zaidi ya 200 mbele,tunapoteza lengo na kuishia kuzua balaa kabla hatujafika hata huko! NHC, nafikiri wameitupa historia yao, ni vema wakumbuke kubadili Act,sio kutoka nje ya lengo kuu.NHC libaki kuwa kimbilio la wanyonge, na sio mkandarasi wa wenye pesa,hao hata msipowajengea watajenga tu, kwani hamuoni?
2)    Watanzania wenzangu, tusilale,hali inabadilika hiyo, tujitahidi kukopa na kujenga. Usiwe kazi kulaumu tu serikali, na wala tusishangae serikali ikiwa inaangalia kwanza wenye PESA, maana hata sisi siku hizi SHIKAMOO inapewa PESA, si majumbani wala makazini. KUBWA ni kujua kuwa “ When you are in the Mess, go to the top of the Mess”, Denzel Washington. Tujiandae kwa kukamata Ardhi kubwa kadri iwezekanavyo,tusing’ang’anie mijini tu, hata vijijini,maana baadae tutakosa pa kulala na ndipo tutanyonywa zaidi. Madenge alisema “Kulala ni bora zaidi ya kula,kwa sababu kula iko ndani ya kulala”,huu ndio wakati aliokuwa akiongelea. WATANZANIA tutafute KULALA kwanza! Wenye nyumba msikubali kuhama, ruhusuni wajenge miji yetu iendelee,ila pamoja na kupewa nyumba sehemu nyingine,pia mpewe kipande cha nyumba sehemu mnayohamishwa,iwasaidie kula. Serikali za mitaa zisimamie hili.
3)    SERIKALI YETU: Chonde chonde, waheshimiwa, MISINGI YA NCHI ISITUPWE, makazi bora ni HAKI YA mwananchi hata kama katiba ya mwanzo haikuweka wazi. Kama kima cha chini 450,000/=,na hivyo mtu huyo anaweza kutoa shilingi 100,000/= kulipa mkopo wa nyumba za NHC, basi msijitoe, mpeni 400,000/=, ili kutimiza 500,000/= wanayoitaka BENKI ili aweze KUPATA NYUMBA mtu wa kima cha chini japo katika hizo nyuma 5000. Na ni vema zikawekwa hasa kwa makundi tunayoyafahamu, kuwa yana kipato cha chini. Mwalimu wa shule ya msingi na Secondary, Manesi, Askari Polisi na Magereza na hata Wafanyabiashara wadogo wadogo. Sio sawa, Serikali kuridhika na NHC inaposema Serikali haitoi Ruzuku kwenye Makazi, na kuendelea kuacha shirika likitumikia na watu wa kima cha juu na kati peke yao (Wachache), ni kutupa haki ya msingi ya Mtanzania. Serikali iagize NHC hata katika mipango yake,iweze kuwasaidia wananchi ambao tayari wana nyumba mijini, hata kama wanahamishiwa sehemu nyingine, iwape makazi katika jengo hilo ili nao wanufaike na urithi wa wazee wao, sio kuwapa pesa na kuwatupia tu mbali,kama ambavyo mara nyingi hufanyiwa, isiwe umasikini wao matajiri wafanye “Opportunity” na serikali imetulia tu. HII INAWEZA KUSAIDIA MAENEO YA MAJENGO,SOKO MATOLA NA GHANA - MBEYA).
4)    Wataalamu,wanazuoni,wanasiasa,wanafunzi vyuoni,Vyombo vya habari na wazalendo wa ukweli! Jamani tuwe na utamaduni wa kuongelea mambo ambayo kweli yanalenga kumkomboa mtanzania bila kuweka itikadi zetu. Sio tu tunakuwa mabingwa wa lawama,kususa, kukata tamaa  na hasa kuilaumu Serikali asubuhi mpaka jioni. Pale inapofanya vizuri, tuongee pia. Serikali huwa inakumbushwa, waliopo mle ni watu kama sisi, wanamapungufu kama sisi na pengine afadhali ya wao! Hivi hii serikali, huwa inafanya mabaya tu? Maana kila kukicha ni lawama tu, na anayesifia tu huyo ni MFUASI wa chama tawala, hii sio sawa. Penye mazuri pia tuseme ndio, hasa ukomavu wa KIFIKRA.

0 comments:

Post a Comment